Habari
Waziri Mhagama Aridhishwa na Ujenzi wa Majengo Tume ya Taifa ya Uchaguzi
Waziri wa Nchi Ofisi ya Wazrii Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa majengo ya Ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi yaliyoko eneo la Njedegwa Jijini Dodoma alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi huo.
Waziri Mhagama amesema hayo alipotembelea Ofisi hizo tarehe 20 Disemba, 2021 kwa lengo la kukagua maendeleo ya ujenzi na kuzungumza na watumishi wa Ofisi za hiyo na kueleza kuwa Ujenzi wa jengo la Ofisi ya Tume ya Uchaguzi ulisaidia Serikali kuja na aina ya michoro itakayoendana na aina ya ardhi iliyopo Dodoma na ujenzi huo umeendana na thamani halisi ya fedha (value for money) ambapo mpaka kuelekea kumaliza ujenzi wa jengo la Ofisi za Tume ya Uchaguzi limegaharimu kiasi cha shilingi Billioni 21.
Aidha Waziri alipongeza jitihada za wakandarasi wa SumaJKT na ARU Consultant kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa jengo la Ofisi ya Tume ya Uchaguzi hadi hatua iliyofikiwa. Ameendelea kuwahimiza Wakala wa Majengo nchini (TBA), kusimamia vizuri kwa kushirikiana na ARU na SumaJkt ili kuhakikisha mapungufu yaliyojitokeza katika mradi yanarekebishwa.
“Tume ya Taifa ya Uchaguzi inategemewa na Taifa zima, kubaki katika ustawi tulionao na hasa katika kutunza Amani na Utulivu, Mshikamano na Umoja ambao umekuwepo katika taifa hili ndani ya miaka 60 ya uhuru na tangu tumeanza kufanya chaguzi zetu,”Alisisitiza
Aliongezea kuwa, Tume ya Taifa ya chaguzi ni Taasisi huru ambayo imewekwa kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania. Taasisi hii inategemewa katika kuhakikisha ustawi wa Taifa unaendelea kuwepo, kwa kuendelea kufuata sheria, taratibu na kuwa wazalendo na waaminifu kwa Taifa.
Amefafanua kwamba wakati wa kupigania Uhuru Sera na mitizamo yote ya Kiutawala na Kiutendaji na Kisiasa na Demokrasia ilikuwa ni kuhakikisha tunapata Uhuru ila baada ya kupata Uhuru ni lazima tuhusianishe kila jambo na maendeleo ya Nchi.
“Mnalo jukumu kubwa sana, katika kazi zenu kila mmoja anapofanya kazi zake aone anadhamana na Tanzania lake", alisema Waziri Mhagama.
Ameeleza kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi ipo kazini muda wote, inapomaliza uchaguzi mmoja inajipanga kwa ajili ya uchaguzi mwingine ikiwa ni pamoja na kuboresha Daftari la wapiga kura. Ametoa rai kwa wafanyakazi wa Tume ya taifa ya Uchaguzi kuendelea kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, taratibu, kanuni na miongozo ambayo Tume ya Taifa ya Uchaguzi inayo na kwa kuzingatia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Naye Mkurugenzi wa tume ya Taifa ya Uchaguzi Dkt. Wilson Mahera Katika taarifa yake amesema ujenzi wa majengo ya tume ya taifa ya uchaguzi unaendelea vizuri na unaelekea kukamilika, umebakiza shughuli ndogo ndogo zinazotakiwa kukamilika tarehe 31 Mwezi Januari 2022 , ujenzi wa jengo la utawala umekamilika kwa 99%, jengo la kuhifadhia vifaa limekamilika kwa 99% na jengo la kutangazia Matokeo ya Uchaguzi ujenzi umekamilika kwa 97%.
=MWISHO=