Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Waziri Mhagama aipongeza Kampuni ya JATU PLC


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama ameeleza kufurahishwa na kasi ya uwekezaji wa wanachama katika kampuni ya JATU PLC na namna inavyowakomboa vijana kuondokana na changamoto zinazowakabili.

Pongezi hizo zilitolewa jana Oktoba 23, 2021 jijini Dodoma na Waziri Mhagama wakati wa hafla ya kuadhimisha miaka 5 ya kampuni hiyo toka ianzishwe mwaka 2016.

Waziri Mhagama amefafanua kuwa, Kampuni ya JATU PLC imekuwa kiuongo muhimu katika kukuza uchumi wa nchi kupitia miundombinu thabiti iliyojiwekea ambayo imejikita katika shughuli za kilimo, viwanda na masoko hivyo zimekuwa ni msaada mkubwa kwa wanachama kuondokana na umaskini.

“JATU PLC ni kampuni iliyoanzishwa na vijana, nafurahi kuona mmeweza kushiriki katika juhudi hizi za Serikali kwa kuhakikisha mnazalisha malighafi na kuongeza thamani ya Mazao mnayozalisha kupitia Viwanda kwa lengo la kuwa na mnyororo wa kuongeza thamani na kulinda ajira za vijana wetu ili kupitia mnyororo huo wa thamani muweze kutoa ajira nyingi na kujipatia kipato,” amesema Waziri Mhagama

“Nipongeze kampuni ya JATU PLC kwa namna imekuwa ikiwasaidia vijana kuondokana na changamoto mbzlimbali zinazowakabili kwa kuwashirikisha katika kilimo, ufugaji na miradi mbalimbali inayoratibiwa na kampuni hiyo maana imewawezesha vijana kuleta mageuzi ya maendeleo katika Taifa lao,” amesisitiza Waziri Mhagama

Aidha amesema kuwa  utafiti wa nguvukazi uliofanyika 2014 ulibainisha asilimia 56 ni vijana hivyo kupitia fursa ya miradi mbalimbali inayotekelezwa na kampuni ya JATU PLC ni vyema ikatumika kuwasaidia vijana kuondokana na changamoto ya ajira kwa kuwashiriki katika miradi ambayo itawaletea matokea yenye tija.

“Serikali itaendela kuhakikisha kuwa inawawekea vijana mazingira mazuri kupitia program zake mbalimbali ambazo zitawawezesha kupata elimu, ujuzi na mitaji ambayo itawasaidia kujiajiri na kuajiri wenzao,” amesema 

“Serikali pia itaendelea kuwasadia vijana wa JATU ili kuhakikisha wanafikia malengo yao,”

Hata hivyo amesema  kuwa, Malengo ya Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Vijana yameainishwa katika nyaraka na miongozo mbalimbali ikiwemo Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano 2020 -2025, Dira ya maendeleo ya Taifa (vision 2025), Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) 2030; Agenda ya Umoja wa Nchi za Afrika 2063; Sera ya Maendeleo ya Viwanda; Sera ya Taifa ya Ajira ya Mwaka 2008

Pia ametoa  rai kwa vijana wote nchini wahitimu wa vyuo vikuu, vyuo vya kati, Sekondari na hata msingi kujiunga katika vikundi na kusajili Kampuni au vikundi vyao ili waweze kusaidiwa kwa urahisi na waweze kutimiza ndoto zao.

“Vijana mnapaswa kuiga kazi nzuri zinazofanywa na vijana wenzenu waliopo JATU PLC. Ili kuliwezesha taifa letu kufikia azma yake ya kufikia uchumi wa kati wa juu,” alisema Mhagama

Aidha ametoa wito kwa vijana hao wa JATU PLC kuwa na nidhamu ya hali ya juu kwani kumekuwa na kasumba ya vijana wengi wakushajulikana na kupata mafanikio kidogo .

” Msipokuwa na Nidhamu mtaanguka  na anguko lenu litakuwa kubwa kuliko  hapa mlipofikia ni muombe Mwenyekiti wa Bodi awasaidie sana kwani nyiyi vijana wa JATU ni mfano mzuri katika jamii,” amesema Waziri Muhagama. 

Katika hatua nyingine Waziri Mhagama amewapongeza  wakezaji katika kampuni hiyo na aliwasihi kuendelea kuongeza mtaji na kupanua wigo wa biashara zao.

Kwa upande wake Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Mizengo Pinda amesema  kuwa kutokana na ukubwa wa kampuni ya JATU PLC ni mafanikio iliyonayo vi vyema vijana wakachangamikia fursa hiyo ili wajikwamue kiuchumi.

“Katika hafla hii tumejifunza mengi kwa kuona kampuni ya JATU PLC inavyotekeleza mikakati yake kwa ufasaha hivyo Vijana mkawekeze JATU,” amesema Mhe.Pinda 

Naye Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mhe. Mwanahamisi Munkunda ametumia fursa hiyo kumpongeza Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama kwa namna ofisi yake imekuwa mlezi mzuri kwa kampuni hiyo ya JATU PLC ambayo imepelekea mafanikio hayo yaliyofikiwa katika miaka mitano.

 Awali  Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya JATU PLC Peter  Gasaya amesema kuwa dira yao  kwa miaka 10 ijayo ni pamoja na Kuanzisha Benki kubwa ya kibiashara

Amesema kuwa  kama jamii ingekuwa na uelewa wakutosha wangekuwa na miradi mingi hiyo ni kutokana na mifumo ya sheria katika ngazi za Serikali za mitaa hasa ngazi za Kata kumekuwa na migongano kuhusu masuala ya kisheria na hivyo kukinzana na kufanya wao kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

“Katika miaka mitano JATU PLC inajivunia mafanikio iliyoyapata ambayo yamewezesha kampuni kufungua rasmi mradi wa Ufugaji, Bima na Bank ambayo itatoa fursa kwa wafugaji na wakulima kutekeleza miradi yao kwa ufanisi na usalama,” amesema Gasaya

Kwa upande wake Katibu  Mkuu JATU Mohamed Simbano amesema kuwa malengo ya JATU ni kuhakikisha wanainua maisha ya kila Mtanzania lishe na usalama wa chakula ambapo kampuni hiyo imeshatoa ajira za kudumu kwa jina 500 na ajira zaidi ya Elfu 10 zisizo za kudumu wa watanzania.

”JATU ni kimbilio la wengi kwani kwasasa kampuni hiyo imejikita katika kilimo na ufugaji ambapo kuanzia  mwaka 2022 hadi mwaka 2023 wataanza kulima mazao ya aina tatu ambayo ni Maharage, Mahindi na Alizeti lakini pia katika kukabiliana na mabadiliki ya tabia ya nchinwameanza kilimo cha umwagiliaji Kiteto.”amesema