Habari
Waziri atoa maagizo 10 kuboresha sekta ya sheria nchini
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa maagizo 10 yanayolenga kuboresha sekta ya sheria nchini na kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa viwango vinavyotakiwa kiutumishi na kitaaluma.
Ametoa maagizo hayo leo (Alhamisi, Machi 21, 2024) wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania uliofanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma.
“Maafisa Sheria pamoja na Mawakili wa Serikali wote nchini tekelezeni majukumu yenu ya kisheria kwa uadilifu, weledi, uwajibikaji, uaminifu, usiri, umakini na kwa kujituma. Pia, Maafisa Sheria na Mawakili wa Serikali nchini kote shirikianeni kikamilifu kutekeleza Kampeni ya Utoaji Msaada wa Kisheria ya Mama Samia. Hakikisheni kuwa kampeni hii inapewa uzito kama mojawapo wa majukumu yenu mahsusi,” amesema.
Maagizo mengine aliyoyatoa ni pamoja na uongozi wa Chama cha Mawakili wa Serikali kushirikiana na Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na watoa huduma wengine kuhakikisha huduma ya msaada wa kisheria inatolewa kwa wananchi wote wenye uhitaji bila ubaguzi wa namna yoyote.
Pia ameitaka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na Taasisi nyingine za utoaji haki wafungue na kuimarisha ofisi zao katika ngazi za chini ili kuhakikisha huduma za kisheria zinafika kwa wananchi wote kwa wakati na bila usumbufu.
“TAMISEMI iratibu Kamati za Mikoa za Kuratibu Huduma za Msaada wa Kisheria ambazo nyingi kwa sasa hazifanyi kazi, ziwezeshwe kifedha na kupewa nyenzo ili ziweze kuwahudumia wananchi katika mikoa yao kwa tija na wepesi,” amesema Waziri Mkuu.
Amesisitiza Wizara ya Katiba na Sheria ishirikiane na Ofisi ya Rais -TAMISEMI kuweka mipango ya kutafuta vyanzo vya fedha ili kuwezesha kamati za mikoa kutekeleza majukumu yake kikamilifu. “Pamoja na kushirikiana na wadau wake wa sheria, ihakikishe watoa huduma wote, bila kujalisha maeneo walipo, wanawezeshwa fedha na nyenzo za kazi na kupatiwa mafunzo ya mara kwa mara ili yawasaidie kutekeleza majukumu yao.”
Ameitaka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iwezeshe upatikanaji wa nakala za miongozo iliyotokana na sheria zote zilizofanyiwa urekebu na ufasiri ili kusaidia watoa huduma za msaada wa kisheria na wananchi kuzielewa na kuzitumia. “Wananchi watumie fursa ya uwepo wa tafsiri za sheria kwa lugha ya Kiswahili ili kufahamu haki zao. Ninawapongeza sana Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kazi ya ufasiri wa sheria za nchi kwa Kiswahili,” amesisitiza Waziri Mkuu.
Kuhusu kusajili kwenye mfumo wao, Waziri Mkuu amesema: “Mawakili wote wa Serikali wajisajili kwenye mfumo wa OAG-MIS. Hii itawawezesha wananchi kuwajua mahali mlipo na kurahisisha upatikanaji wa huduma za sheria mbalimbali. Mahitaji makubwa ya wananchi yanahusiana na upatikanaji wa elimu katika utatuzi wa migogoro kwenye makosa ya jinai, ndoa, ardhi, kazi na mirathi. Hivyo basi, wekeni mkakati mahsusi wa kuendelea kuelimisha wananchi katika maeneo hayo.”
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema anatambua jitihada za uotoaji huduma za kisheria zinazofanywa na Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, asasi za kiraia, taasisi za umma na binafsi zikiwemo Chama cha Wanasheria Tanganyika, Legal and Human Rights Centre (LHRC), Tanzania Legal Aid Providers (TANLAP), Legal Service Facility (LSF), Tanzania Human Rights Defenders Coalition (THRDC), UNDP, UN Women, Polisi na Magereza.
“Vilevile, ninatambua mchango mkubwa wa watoa huduma za msaada wa kisheria, na makundi mengine yote katika kutoa huduma za kisheria. Niwahakikishie kwamba Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kutoa ushirikiano wa dhati kwa wadau wote wa utoaji huduma za kisheria.”
Amesema Serikali itaendelea kutoa rasilimali muhimu ili kuziwezesha taasisi hizo zitoe huduma kwa ufanisi. “Kundi hili kubwa la Maafisa Sheria na Mawakili wa Serikali limebeba dhamana kubwa ya kutoa huduma za kisheria. "....nendeni mkaitendee haki dhamana hii kubwa kwa ustawi wa wananchi wa Tanzania,” amesisitiza Waziri Mkuu.
Kwa upande wake, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Dkt. Eliezer Feleshi amesema mkutano huo ni jukwaa la kitaaluma la wanasheria wa umma ambao hufanyika mara moja kwa mwaka kwa lengo la kuwapa fursa kujadili maendeleo ya sekta ya sheria.
“Lengo kubwa ni kukuza ufanisi wa wanachama, kujenga uelewa kuhusu maendeleo ya huduma za kisheria na kuwawezesha kutathmini mafanikio na changamoto wanazokutana nazo katika taasisi zao. Ofisi yangu itaendelea kufanya kila linalowezekana ili kuwezesha kuyafikia matarajio ya chama hiki,” alisema Jaji Dkt. Feleshi wakati akielezea lengo la mkutano huo.
“Mawakili wa Serikali tutaendelea kutumia mifumo na miongozo kuhudumia wananchi wote nchini. Kila mmoja anawajibika kuweka mikakati madhubuti katika kuitekeleza kaulimbiu yetu kwa weledi, hasa kuwafikia wananchi wasio na uwezo.” Kaulimbiu ya mwaka huu inasema: “Upatikanaji wa Huduma za Kisheria kwa Wananchi ni Nguzo Muhimu kwa Ustawi wa Jamii."