Habari
Wazalishaji wa mbegu Mkalama waomba serikali kuimarisha ufungashaji
Wazalishaji wa mbegu za alizeti katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, mkoani Singida, wameiomba Serikali kuongeza juhudi katika kuwawezesha kuandaa vifungashio bora vya mbegu ili kuongeza thamani ya mazao yao sokoni.
Wito huo umetolewa wakati wa ziara ya ujumbe wa Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) kwa kushirikiana na wawakilishi kutoka IFAD katika Kijiji cha Ilunda, waliokuja kufuatilia utekelezaji wa programu hiyo.
Bw. Athumani Ramadhani, mzalishaji wa mbegu aina ya Record, alisema: “Tunaomba Serikali itupe msaada wa kitaalamu kuandaa vifungashio bora vitakavyotangaza mbegu zetu na kuongeza thamani sokoni.”
Naye Bi. Aziza Ramadhani aliongeza kuwa uzalishaji huo umeimarisha ushirikiano wao na taasisi za Serikali kama ASA na TOSCI, zinazopima ubora kabla ya mbegu kuingia sokoni.
Kwa Upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mkalama, Bi. Asia, alisema Serikali inalenga kuifanya Mkalama kuwa mfano bora katika utekelezaji wa Programu ya Kilimo na Uvuvi (AFDP), huku akisisitiza umuhimu wa kuongezwa nguvu katika sekta hiyo.