Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Wanawake wachangia 35% ya Pato la Taifa


Wanawake nchini Tanzania wanatajwa kuchangia sehemu kubwa ya Pato la Taifa. Takwimu zinaonesha kuwa, zaidi ya 35% uchumi wa Tanzania hutokana na jitihada, juhudi na jasho la wanawake. Ambapo katika sekta mbalimbali za uzalishaji mali asilimia 70 ya nguvu kazi ya kilimo ni wanawake hasa katika mazao ya chakula.

Mchango wa mwingine wa wanawake unajidhihirisha katika biashara, viwandani na katika huduma za kifedha kupitia utafiti uliofanywa na Chama cha Mabenki Tanzania (TBA) mwa ka 2022 umeonesha wanawake ni 47% ya wafanyakazi wote wa sekta ya fedha. Pia wanashika 10% ya nafasi za kufanya maamuzi. Vile vile, 18% wakiwa wajumbe katika bodi za wakurugenzi sawa na wastani wa wanawake wawili katika kila bodi.

Hayo yamebainishwa leo Aprili 14, 2025 jijini Dodoma na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko wakati aliposhiriki katika ufunguzi wa Mkutano wa mwaka wa Chama cha Wanawake katika Sekta ya Fedha (TAWiFA).

Pamoja na mafaniko hayo, Dkt. Biteko ametaja changamoto zinawakabili wanawake katika sekta ya fedha kuwa ni uhaba wa upatikanaji wa mikopo yenye riba nafuu, elimu duni ya masuala ya kifedha na uchache wa nafasi za kushiriki katika maamuzi ya Sera za Fedha.

Akizungumzia namna tamaduni, mila na desturi zinavyoweza kuwa changamoto kwa wanawake, amewataka wanawake nchini kuzingatia misingi ya malezi kwa watoto wao kwa kuwapa nafasi sawa watoto wa kike na wa kiume ili suala la usawa wa kijinsia lisiwepo badala yake iwe uwezo wa mtu yeyote kufanya kazi.

“ Kwa kushirikiana na wadau wengine Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Mhe.  Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za makusudi ili kutatua changamoto zinazomkabili mwanamke na hivyo kuchochea maendeleo yake,” amesema Dkt. Biteko.

Amebainisha baadhi ya hatua hizo kuwa  ni kuwaamini na kuwapa wanawake nafasi za juu za uongozi na hivyo kuwepo katika kufanya maamuzi, kufanya Mapitio na Tathmini ya Utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Jinsia na Maendeleo ya Wanawake ya mwaka 2000,  kuandaa miongozo mbalimbali ikiwemo  Mwongozo wa Ulinzi na Usalama wa Wanawake na Vijana Vyuoni uliozinduliwa mwaka 2023 na kutoa fursa nyingine mbalimbali za kifedha na kiuchumi kwa wanawake.

Amesisitiza “Naomba hapa nitoe rai kwenu kuwa, mkiwa mnaendelea kutekeleza majukumu yenu, msisahau kuhusu kuwekeza katika teknolojia. Maana Dunia ya sasa inazidi kwenda zaidi katika maisha ya kidigitali. Hii itasaidia kurahisisha biashara na kufikisha huduma kwa wepesi hususan katika maeneo ya vijijini,”

Fauka ya hayo, Dkt. Biteko amesema kupitia mijadala na maazimio yatakayotolewa katika kikao hicho, itapatikana  mbinu mpya za kuongeza ushiriki wa wanawake katika sekta ya fedha na uchumi wa nchi kwa ujumla kupitia mabenki, kampuni za bima, masoko ya mitaji. Pamoja na mbinu na njia mbalimbali za fedha mtandao zinazotatua changamoto zinazomkabili mwanamke katika sekta ya fedha.

Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha, Mhe. Hamad Chande amewapongeza wanawake nchini kwa kuanzisha Chama hicho kinacholenga kusaidia wanawake kiuchumi.

Amewahakikishia “ Serikali imeweka mazingira wezeshi kwa kutunga sera na sheria za kiuchumi ili wanawake na makundi mbalimbali yaweze kuimarika kupitia taasisi na vyama kama hivi. Aidha, Serikali itaendelea kushirikiana nanyi ili kuimarisha TAWiFA ili kuhakikisha nafasi ya mwanamke inazidi kuwa juu katika jamii.”

Rais wa Chama cha Wanawake katika Sekta ya Fedha (TAWiFA), Fikira Ntomola amesema kuwa wanawake nchini wameendelea kujishughulisha ili kuhakikisha sekta ya fedha nchini inakuwa. Aidha, jamii inapaswa itambue uwekezaji kwa wanawake si hisani bali ni uwekezaji wa kimkakati kwa maendeleo ya Taifa.

“ Tunaahidi kufikisha elimu ya fedha kwa wanawake katika maeneo mbalimbali  nchini kwa kuandaa mafunzo na warsha kwa lengo la kuongeza uwezo wa kusimamia masuala yao ya fedha na biashara,” amesema Bi. Ntomola.

Ameongeza kuwa TAWiFA imedhamiria kuleta mabadiliko chanya kuhusu ushiriki wa wanawake katika sekta ya fedha, aidha wanaishukuru Serikali kwa kuendelea kuweka sera na sheria zinazochochea uchumi jumuishi  na uwepo wa usawa wa kijinsia kiuchumi na kijamii.

“Tumekuwa tukiwajengea uwezo wanawake wa kuendesha biashara zao kiufanisi, kukuza biashara zao na kupanua  wigo wao kuhusu sekta ya fedha,” amebainisha Bi. Ntomola.

Amewaomba wadau mbalimbali nchini kufungua milango ya fursa kwa wanawake, na kuwa TAWiFA ipo tayari kushirikiana nao kwa ajili ya kutoa elimu ya fedha kwa umma, pamoja na tafiti za kuendeleza miradi ya kusaidia wanawake ili kujenga sekta ya fedha iliyo jumuishi.

Makamu wa Rais wa Chama cha Wanawake katika Sekta ya Fedha (TAWIFA), Nangi Massawe amesema kuwa Chama hicho kinakutanisha wanawake katika sekta ya fedha ili kujenga sekta yenye usawa kwa manufaa ya Taifa.

TAWiFA ina jumla ya wanachama 204 na kimeendelea kuhakikisha wanawake wanashiriki katika sekta hiyo ili kuchochea maendeleo.

MWISHO