Habari
Wananchi waaswa kuwaunga Mkono Watu Wenye Ulemavu
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuwaunga mkono Watu Wenye Ulemavu ili kuendelea kuvumbua vipaji vyao katika maeneo mbalimbali.
Naibu Waziri ametoa wito huo leo Jijini Dodoma katika Ukumbi PSSSF wakati wa uzinduzi wa Msimu wa Pili wa Mashindano ya kusoma Quran kwa Watu Wenye Ulemavu yaliyoandaliwa na Taasisi ya Lulida.
Ameeleza kwamba, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kushirikiana na Wenye Ulemavu bega kwa bega ili kuhakikisha masuala mbalimbali yanayowahusu yanapewa kipaumbele.
“Nipo kwenye hatua ya kupita katika makundi mbalimbali ili kusikiliza changamoto na kuweka mikakati ya muda mrefu na muda mfupi katika kuzifanyia kazi,” alisema Naibu Waziri Nderiananga.
Aidha, aliongeza kusema, “nimefurahishwa na taasisi ya Lulida kwa kuanzisha jambo hili kwa sababu ni sehemu ya kujali Watu Wenye Ulemavu kuona vipaji vyao na vipawa vyao”.
Naye Mwenyekiti wa Taasisi ya Lulida Mhe. Hajjat Riziki Lulida ametoa rai kwa vyombo vya habari kuendeleza upendo na kujikita katika kuandika habari zenye kujenga misingi ya umoja na ushirikiano kwa jamii.




