Habari
Walimu tujiendeleze kuendana na mabadiliko duniani – Dkt. Biteko
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewahimiza walimu nchini kujiendeleza kitaaluma ili kuendana na mabadiliko yanayoendelea kutokea duniani.
Dkt. Biteko amesema hayo Oktoba 16, 2025 katika Manispaa ya Musoma, mkoani Mara wakati akifungua Semina ya Viongozi wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) kanda ya Ziwa na Ziwa Magharibi iliyoshirikisha viongozi kutoka mikoa minane.
Amesema Serikali imekuwa ikiboresha maisha ya watumishi wake wakiwemo walimu na tayari na walimu wenyewe wanaelewa maboresho yaliyofanyika ili kuwawezesha kuishi maisha ya staha.
“Rais wa CWT amesema hapa kwamba viongozi wote ni wapya, wanafanya kazi wakiwa wapya na muhimu kufanya kazi mkiwa wapya kwa kuzingatia kuwa Dunia imebadilika,” amesema na kuongeza kuwa “Mimi ni zao la mwalimu na nimetumikia taaluma hii, tulikuwa tunadai mambo kama haya yenye kulenga kuboresha hali za walimu tangu kipindi hicho na hata sasa niwahakikishie kuwa mnayoyaomba hayaanguki katika masikio yaliyokufa, serikali imeyasikia,” amesema Dkt. Biteko
Ameendelea “Kusema kweli Serikali imefanya mambo mengi kuboresha hali ya walimu na inaendelea kufanya kila jitihada kuhakikisha maisha yao yao yanakuwa bora, Wakati tukiendelea kudai maslahi tukumbuke kwamba dunia imebadilika sana. Pia tuseme ukweli na pengine kutoa shukrani kwa yale mazuri yaliyotokea ama kufanyika”
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita kwa kushirikiana na wadau imeendelea kuboresha miundombinu ya shule na rasilimali mbalimbali ili kutekeleza miradi tofauti tofauti.
Aidha, amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameahidi kutoa ajira zaidi ya 7000 kwa walimu wa masomo ya Hisabati na Sayansi ndani ya kipindi cha siku 100 atakapokuwa amechaguliwa kuwa Rais kwa kipindi kingine cha miaka miaka mitano.
Vilevile amewataka walimu kutumia haki yao kikatiba kujitokeza kupiga kura, kuwachagua viongozi wao ifikapo tarehe 29 Oktoba, 2025 ili kutimiza haki na wajibu wa kidemokrasia.
“Hakuna nchi inaweza kuwapata viongozi wa kidemokrasia bila kuwachagua kwa kuwapigia kura. Nawakumbusha ikifika siku ya uchaguzi mkawachague viongozi ambao pamoja na kutimiza jukumu la kikatiba, itakuwa inawapa uhalali wa kudai maendeleo” amesema Dkt. Biteko.
Naye Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi amesema Serikali ya awamu ya sita chini ya Uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya maboresho katika kada ya ualimu ikiwa ni pamoja na kuboresha maslahi ya walimu nchini.
Kwa upande wake Rais wa CWT taifa, Dkt. Suleiman Ikomba ameiomba Serikali kukifanya chama hicho kuwa tumaini lake na kuwaona walimu kama watu muhimu ili kuwajengea heshima kwa jamii.
Amefafanua kuwa CWT kama chama cha kitaaluma inaamini kwamba demokrasia ni suala lisiloepukika katika kuwaletea watu maendeleo hivyo, kuahidi kwenda kupiga kura ifikapo Oktoba 29, 2025.
Awali katika Risala ya CWT, wameiomba Serikali kuwapa posho ya kufundishia, posho ya nauli na kulipa madeni ya walimu ya likizo na uhamisho pamoja na stahiki kwa wakuu wa Idara.
Pia Chama hicho kimemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hatua mbalimbali zilizochukuliwa ikiwa ni pamoja na nyongeza ya mishahara, kupandishwa vyeo, kupandishwa vidato, madaraja na kupewa mserereko kwa waliotakiwa kufanyiwa hivyo.
Semina hiyo iliyobeba Kauli mbiu Uchaguzi Mkuu ni Jukumu letu walimu kushiriki Uchaguzi Mkuu Oktoba, 2025 imeshirikisha zaidi ya walimu 470 kutoka mikoa ya Mara, Simiyu, Mwanza, Shinyanga, Geita, Kigoma, Tabora na Kagera.
Mwisho.