Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Wadau waombwa kushirikiana na Serikali kukabiliana na utapiamlo


Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi ametoa rai kwa wadau wa sekta binafsi kushirikiana Serikali katika kukabiliana na suala la utapiamlo nchini.

Ametoa kauli hiyo Jijini Dar es Salaam wakati kikao kilichohusisha wadau wa sekta binafsi katika kujadili maandalizi ya Mkutano wa 10 wa lishe unaotarajiwa kufanyika Jijini Mwanza Mwezi Septemba mwaka huu.

Dkt. Yonazi amesema biashara inahitaji watu wenye uwezo wa kufikiri haraka katika hatua za ukuaji wa kiuchumi, ili fikra hizo ziendelee tunahitaji kujenga Jamii bora.

“Lazima tuunganishe nguvu katika kukabilina na changamoto ya udumavu katika Jamii yetu ili tuweze kuwa na jamii yenye afya bora,” alisema

Aliongezea kuwa sekta binafsi imepata nafasi ya kutambulika na kushikana mkono na Serikali katika kukabiliana na changamoto ya udumavu nchini.

“Tunahitaji kuwa na   taifa lenye watu wenye afya nzuri, siha njema wanaoweza kufikiri, wanaoweza kuweka mikakati na kuongeza ushawishi wa kibiashara nje ya mipaka ya nchi yetu,” alisema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Dkt. Germana Leyna amesema sekta binafsi inayo nafasi ya kuhamasisha walaji katika kujenga hamasa ya kuleta mabadiliko chanya katika lishe kulingana na bidhaa zinazozalishwa.

“Tatizo la utapiamlo lisipopatiwa ufumbuzi, linaweza likapunguza nguvu ya ununuaji hata kama bidhaa zitakuwa bora na muhimu,”Dkt. Germana

Naye Bw. Ally Sechonge kutoka kampuni ya Tanga Freshi amesema kwa mujibu wa takwimu za Bodi ya maziwa ni 4% ya Maziwa yanayotoka kwa Ng'ombe ndio yanayosindikwa na 96% yananywewa bila kusindika.

 “Tatizo kubwa ni kwamba walaji wanakuwa na maamuzi jinsi gani watatumia fedha yao, bila kuzingatia  swala la  utaratibu mzuri wa kula,” alisema.

Naye Bw. Iddi Mvungi kutoka Kampuni ya Bakhresa ameishukuru Serikali kwa kujumuisha sekta binafsi katika mapambano dhidi ya utapiamlo.

“Tunapenda kuihakikishia serikali kwamba tutaendelea kushirikiana nayo katika  kuhakikisha maelekezo yote yanayoelekweza tunayazingatia katika katika uzalishaji wa bidhaa zetu,”Alisema

=MWISHO=