Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Wabunge wa Taifa la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo waridhishwa na utekelezaji wa Mji wa Serikali Mtumba


Wawakilishi wa Bunge la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wameridhiswa na utekelezaji wa ujenzi wa Mji wa Serikali walipofanya ziara leo Mei16,2026 Mtumba,Jijini Dodoma.

Akizungumza wakati wa Ziara hiyo, Kiongozi wa msafara kutoka DRC, Mhe. Prof. Willy Mishiki (Mb) ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia na kutekeleza Mradi huu, pia ameshukuru kwa kiwanja kilichopatiwa Ubalozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwaajili ya ujenzi wa ofisi za balozi.

Ameongeza kuwa, mradi huu umewafungua macho wao kama Wabunge kwani watakwenda kushauri na kuamsha hali ya Serikali yao kutimiza maono ya Hayati Patrice Lumumba ya kuhamia katika Mji wa Kananga, kwakua mji huo upo  katikati ya Kongo, hali itakayosaidia pia kupunguza msongamano katika Mji wa Kinshasa wenye makadirio ya watu Milioni 20.

Aidha, ameomba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuipa ushirikiano Nchi yao wakati watakapo anza utekelezaji wa ujenzi wa mji wao wa Serikali kwa kuwapa Wataalamu na Taasisi zilizoshiriki ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba kwaajili ya  kuwajengea uzoefu.

Awali, akiukaribisha Msafara huo, Balozi wa Tanzania katika Jamhuri  ya Kidemokrasia ya Kongo, Mhe. Said Juma Mshana ameupongeza Msafara huo kwa uamuzi waolioufanya wa kutembelea Mradi huu na kuwahimiza wakaishauri Serikali yao kuitumia Fursa ya kiwanja walichopatiwa kutekeleza ujenzi wa Balozi yao katika Mji huu wa Serikali.

Naye, Mratibu wa Mji wa  Serikali wa Mtumba kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu-Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu Bw. Noel Mlindwa, amesema kuwa malengo ya Serikali kuhamia Dodoma ni pamoja na kusogeza Huduma katikati ya Nchi ili kuwezesha wananchi wa maeneo mbalimbali kufika kwa urahisi zaidi.

Ameongeza kuwa, jumla ya majengo ya kudumu 17 kati ya 34 yalioyojengwa katika awamu ya pili yamekamilika na yameanza kutumika rasmi na baadhi yanaendelea kujengwa yakiwa katika hatua za ukamilishaji huku wastani wa ukamilishaji wa majengo ya wizara imefikia asilimia 96. Aidha, amepongeza juhudi zinazofanywa na Seriikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuhanisha Makao Makuu kutoka Kinshasa na kuhakikisha kuwa wataalamu wetu watakua tayari kutoa ushirikiano ikiwemo uzoefu ili kufanikisha mpango huo.

 

=MWISHO=