Habari
Vijana Wahamasishwa Kuwekeza Katika Shughuli za Kiuchumi
Vijana nchini wahamasishwa kuwekeza kwenye shughuli za kiuchumi ili kuondokana na changamoto ya ukosefu wa ajira kwa kuanzisha miradi au shughuli za uzalishaji mali zenye tija zitakazowawezesha kuchangamkia na kusimamia ipasavyo fursa mbalimbali za kukua kiuchumi na kuchangia pato la taifa.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Kaspar Mmuya ameyasema hayo Januari 6, 2022 wakati wa Ufungaji wa Mafunzo ya Ujasiriamali na Usimamizi wa Biashara kwa vijana katika Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara.
Naibu Katibu Mkuu alieleza kuwa, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu inasimamia utekelezaji wa afua za kushughulikia mahitaji ya makundi maalum ya vijana wakiwemo vijana kutoka jamii ya wafugaji kama ilivyoanishwa kwenye Ibara ya 3.25 ya Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya Mwaka 2007, hivyo kupitia afua hiyo vijana hupatiwa mafunzo ya ujuzi tepe kulingana na mahitaji yao ambapo huhamasishwa kuunda vikundi vya uzalishaji mali na kuunganishwa kwenye fursa za uwezeshaji vijana kiuchumi kupitia asilimia 4% ya mapato ya Halmashauri na Mfuko wa Taifa wa Maendeleo ya Vijana.
“Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua mchango wa vijana katika kukuza uchumi wa nchi, hamasa kubwa imekuwa ikitolewa na viongozi kwa vijana wazawa kuanzisha viwanda, makampuni na shughuli mbalimbali za uzalishaji mali zenye tija zitakazowafanya wanakuwa kiuchumi na kujiletea maendeleo katika jamii zao,” alisema Naibu Katibu Mkuu Mmuya
“Hapa Kiteto mnaongoza kwa uzalishaji wa mahindi bora na alizeti, hiyo ni fursa kwenu vijana kuanzisha viwanda vidogo vidogo vitakavyo zalisha bidhaa zinazotokana na mazao hayo,” alisema
Alifafanua kuwa, Serikali inatambua vijana ni kundi kubwa linalofanya nguvukazi ya taifa, kwa mujibu wa taarifa za Shirika la takwimu la Taifa (NBS) inakadiriwa kuwa idadi ya vijana nchini ni Milioni 17.7 sawa na ailimia 31.5% ya Idadi ya watu wote nchini ambapo kati ya vijana 17.7 vijana wenye uwezo wa kufanya kazi ni Milioni 14.2 Sawa na asilimia 80.3% (Ripoti ya Matokeo ya utafiti wa Nguvu Kazi ya mwaka 2020/2021).
“Asilimia kubwa ya vijana wanaishi vijijini ambapo wanajishughulisha na kilimo na ufugaji katika kuendesha Maisha yao, hivyo kutokana na takwimu hizo, Serikali imedhamiria kuendelea kuboresha mazingira katika sekta ya kilimo na ufugaji ili vijana wengi waweze kushiriki kikamilifu katika kukuza uchumi na kujiletea maendeleo,” alieleza Mmuya
Aliongeza kuwa lengo la mafunzo haya ni kubadilisha mitazamo ya vijana katika kuchangamkia fursa mbalimbali za kuichumi ndio maana mwitikio wa vijana katika Halmashauri ya Kiteto kushiriki mafunzo hayo ni mkubwa sana.
“Katika Mkoa huu wa Manyara, Halmashauri ya Kiteto ambapo mafunzo haya yamefanyika vijana wameonesha uhitaji mkubwa wa kupatiwa mafunzo haya. Hali hii inaashiria kuwa mafunzo haya yatakuwa chachu kwa vijana kushiriki katika shughuli za kiuchumi kwa mafanikio na tija.
Aidha, Naibu Katibu Mkuu Mmuya alitumia fursa hiyo kuhimiza Halmashauri zote nchini kuwezesha vijana kiuchumi kupitia kupitia mikopo inayotolewa kwa Vijana asilimia 4%, Wanawake asilimia 4% na Watu wenye Ulemavu asilimia 2%.
Sambamba na hayo aliwataka Maafisa Maandeleo ya Vijana na Maafisa Maendeleo ya Jamii kuweka mifumo na utaratibu mzuri wa ufuatiliaji wa vikundi vya vijana vinavyopatiwa mikopo na Halmashauri ili kupata matokeo yenye tija ya maendeleo ya fedha hizo za serikali zinazotolewa moja kwa moja kwa wananchi. Pamoja na hayo amewataka vijana kutumia fursa hiyo kujifunza kwa umakini mkubwa ili muweze kupata maarifa na ujuzi utakaowasaidia katika kuendesha miradi yenu na kujikwamua kiuchumi.
Pia, Naibu Katibu Mkuu Mmuya alishukuru Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA) kwa kuendelea kusaidia jitihada za Serikali katika kutekeleza programu mbalimbali za Maendeleo ya vijana nchini.
Awali Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw. Julius Tweneshe alisema kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuyafikia na kuyawezesha kiuchumi makundi yote ya vijana yanayojumuisha waliopo mijini, vijijini, wenye mahitaji maalumu ikiwemo vijana wa kike na kiume, Vijana wanaotoka katika jamii za wakulima na wafugaji na vijana wanaoishi katika mazingira hatarishi.
“Serikali kupitia Idara ya Maendeleo ya Vijana tumeweka mikakati ya kuwasaidia vijana kwa kuhakikisha kuwa tunayafikia makundi yote maalumu ya vijana likiwemo kundi lenu hili la vijana kutoka kwenye Jamii ya Wafugaji,” alisema
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo ya Kiteto, Bi. Beatrice Rumbeli ambaye ni Afisa Mipango alisema kuwa halmashauri hiyo imefanikiwa katika shughuli za kuwezesha wananchi kiuchumi ikiwemo kutoa mikopo kwa vikundi vya Vijana, Wanawake na Wenye Ulemavu.
“Katika Mwaka wa fedha 2021/2022 Halmashauri ya Kiteto ilitenga kiasi cha shilingi milioni 183 kupitia mapato ya ndani kwa ajili ya kuwezesha vikundi vya Vijana, Wanawake na Wenye Ulemavu ambapo hadi sasa jumla ya milioni 120 zimekwisha tolewa kwenye vikundi,” alieleza Rumbeli
Naye Kijana Mnufaika wa Mafunzo hayo Bw. Marisix Urasa, aliishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuwapatia mafunzo hayo ya ujasiriamali na usimamizi wa biashara yaliyoanza kutolewa katika Halmashauri hiyo ya Kiteto kuanzia tarehe 04 hadi 06 Januari, 2022 ambapo alieleza kuwa mafunzo hayo yatakuwa ni chachu kwa vijana katika wilaya hiyo kubadilika kifikra kwa kuanza kurasimisha na kuboresha biashara zao.
“Sisi vijana wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto tunatambua Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasimamia utekelezaji wa Awamu ya Tatu ya Mpango wa Kitaifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano kuhusu kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, hivyo sisi vijana kama nguvukazi ya Taifa tunao mchango mkubwa katika kufanikisha jitihada hizo za Serikali na za Viongozi wetu wa nchi ili kufikia malengo ya mpango huo,” alisema Urasa