Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Thamani ya mikopo TADB imefikia bilioni 317-Majaliwa


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema thamani ya mikopo inayotolewa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imeongezeka kutoka shilingi milioni 776 mwaka 2015 hadi shilingi bilioni 317 Juni mwaka 2023.

Mheshimiwa Majaliwa amesema mafanikio makubwa ni azma ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwainua wakulima wa Tanzania na kuendeleza Sekta ya Kilimo kwa ujumla.

Amesema hayo leo (Alhamisi Julai 06, 2023) wakati alipozindua Ofisi ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania katika Kanda ya Kusini, Mtwara.

“Ukuaji huo umechagizwa na ongezeko la mtaji  kutoka shilingi bilioni 61.09 mwaka 2015 hadi shilingi bilioni 302.01 katika mwaka 2022.Ninawapongeza sana kwa hatua hiyo kwani kadri mtaji unavyoongezeka na uwezo wa kuhudumia wakulima kwa njia ya mikopo unaongezeka”

Akizungumza baada ya uzinduzi wa Ofisi hizo Mheshimiwa Majaliwa amewataka wananchi wa mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma kuchangamkia fursa ya uwepo wa Ofisi hiyo ya Kanda Mtwara kupata uelewa  zaidi kuhusu utaratibu wa kupata mikopo. “Nendeni mkakope ili mpate vifaa vya kisasa na kupata tija kupitia kilimo”

“Menejimenti ya Benki na watumishi wa Ofisi ya Kanda ya Kusini  wekeni masharti nafuu katika kutoa mikopo ili kuwezesha mikopo kwa wakulima, wavuvi na wafugaji kwa wakati”

Katika Hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amesema Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania imetenga shilingi bilioni 35 kwa ajili ya mpango wa kuwakopesha wakulima wa korosho ili kuendeleza zao hili. “Ni matumaini yangu kwamba fedha hizi na nyingine ambazo mtaendelea kuwekeza huko zitajikita katika kufanikisha malengo”

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Hamad Hassan Chande ni amesema kuwa uzinduzi wa Ofisi ya TADB Kanda ya Kusini ni ushahidi tosha wa dhamira ya dhati ya Serikali ya kuhakikisha kuna kuwa na upatikanaji wa mitaji kupitia taasisi za fedha na ni kielelezo cha utekezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Taifa.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Frank Nyabundege amesema lengo la kufungua Ofisi katika Kanda ni kuhakikisha wanafikia wakulima wengi zaidi ambapo mpaka sasa TADB imefungua ofisi sita katika Kanda Ziwa, Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Magharibi, Kanda ya Kati na Kanda ya Kusini

Ameongeza kuwa kupitia uzinduzi wa Ofisi hiyo wataweza kufikia wakulima, wafugaji na wavuvi kwenye mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma. “Tutatoa huduma za kibenki zinazoweza kupatikana kwa urahisi, kama vile mikopo ya kilimo, ujenzi wa viwanda na maghala, mikopo ya matrekta na mashine zingine za kisasa, pamoja na ushauri wa kitaalamu”