Habari
TGPA Yapokea ugeni wa wachapishaji kutoka uganda kuimarisha ushirikiano
Wakala wa Serikali wa Uchapishaji Tanzania (TGPA) leo umepokea ugeni wa watu 24 kutoka Shirika la Uchapishaji la Uganda (Uganda Printing and Publishing Corporation – UPPC) waliowasili nchini kwa ziara ya kikazi yenye lengo la kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushirikiano katika sekta ya uchapishaji wa serikali.
Ujumbe huo umeongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa UPPC, Profesa Joackim Buwembo, ukijumuisha wajumbe wa bodi, Mpigachapa Mkuu wa Serikali ya Uganda, Profesa Sudi Nangoli, pamoja na watumishi kutoka idara mbalimbali za shirika hilo.
Kwa mujibu wa taarifa za TGPA, ziara hiyo imelenga kujifunza na kubadilishana uzoefu katika uchapishaji wa nyaraka za serikali, hususan Gazeti la Serikali, pamoja na uchapishaji wa nyaraka zenye alama za usalama (security printing).
Katika ziara hiyo, pande zote mbili zimefanya vikao vya kitaalamu na majadiliano yaliyolenga kuimarisha mifumo ya uchapishaji, kuongeza ubora wa huduma na kuzingatia viwango vya usalama katika uchapishaji wa nyaraka nyeti za serikali.
Aidha, TGPA na UPPC zimekubaliana kushirikiana katika maeneo ya uchapishaji, kuandaa mafunzo kwa watumishi wao, pamoja na kuanzisha utaratibu wa kubadilishana uzoefu kwa lengo la kuongeza ufanisi na kuimarisha mahusiano ya kitaasisi kati ya Tanzania na Uganda.
Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za taasisi hizo kuendeleza ushirikiano wa kikanda katika sekta ya uchapishaji wa serikali na kuhakikisha huduma bora zinatolewa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa




