Habari
TANZANIA YAZINDUA KAMPENI YA UELEWA KUHUSU MAJANGA KITAIFA
* Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kutoa tamko la Serikali siku ya kilele cha maadhimisho hayo kimataifa Oktoba 13
KAMPENI Ya elimu kwa Umma kuhusu uelewa wa masuala ya maafa imezunduliwa rasmi leo Oktoba 7 hadi siku ya kilele Oktoba 13 ambapo ulimwengu utaadhimidha siku hiyo kwa ajili ya kukuza utamaduni wa usimamizi wa maafa kimataifa na kitaifa ili kuzuia na kupunguza madhara ya majanga pamoja na kujiandaa katika kuyakabili na kurejesha hali katika ubora zaidi baada ya majanga hayo kutokea.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo leo jijini Dar es Salaam Katibu mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu; Sera, Uratibu, Bunge, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Tixon Nzunda amesema maadhimisho hayo ya kitaifa yamejikita katika utoaji wa elimu kwa umma ili kuhakikisha jamii inatambua aina ya majanga na vyanzo vyake, madhara ya maafa, kupunguza athari zake na namna ya kujiandaa katika kuyakabili na tamko rasmi la Serikali litatolewa siku ya kilele na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa.
Nzunda amesema kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni;
"Kwa Umoja Wetu... Tunaweza Kuokoa Dunia." Ni fursa kubwa ya kutambua umuhimu wa ushirikiano baina ya Serikali na wadau wa kimataifa katika hatua za kuzuia na kupunguza hatari na madhara ya maafa katika mifumo ya maisha, afya, uchumi, elimu, jamii, utamaduni, miundombinu na mazingira.
Amesema kuwa elimu hiyo ya uelewa kwa umma kuhusiana na majanga itatolewa kwa njia mbalimbali ikiwemo maelezo ya ana kwa ana kwa wananchi, vipindi vya luninga, redio, vipeperushi vya ufafanuzi wa maafa na hatua za kuchukua pamoja jumbe katika mitandao ya kijamii.
"Maonesho ya wazi yatafanyika katika viwanja vya Mazania, Chato Mkoani Geita kuanzia Oktoba 9 hadi 13 mwaka huu, Dodoma yatafanyika katika viwanja vya Nyerere Square kuanzia Oktoba 11 hadi 13 na vipindi vya redio na luninga vitafanyika kuanzia leo hadi siku ya kilele Oktoba 13 na wataalam mbalimbali watatoa elimu katika sekta mbalimbali ikiwemo maafa, hali ya hewa, kilimo, ardhi, nishati, Zima moto, shirika la Msalaba Mwekundu Tanzania, mashirika ya kimataifa na Umoja wa mataifa, Asasi za kiraia na vyuo vikuu." Amesema.
Nzunda amesema, Serikali imeandaa mpango wa kukabiliana na maafa katika halmashauri 20 na kwa kuzingatia wajibu wa sekta katika usimamizi wa maafa na huduma za kibinadamu imeandaa mpango na miongozo ya kujiandaa na kukabiliana na maafa katika sekta mbalimbali ikiwemo mpango wa kukabiliana na dharura katika sekta ya afya, mwongozo wa huduma ya msaada wa kisaikolojia na kijamii kwenye maafa, mpango wa dharura wa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko kwa sekta ya usafiri wa anga, mpango wa dharura wa kujiandaa na kukabili mlipuko wa virusi vya Ebola pamoja na mwongozo wa utendaji wa kituo cha operesheni na Mawasiliano ya dharura.
Vilevile ameeleza kuwa Serikali itaendelea kuboresha Sera, Sheria na kuandaa mikakati kwa lengo la kuimarisha mfumo wa uratibu na usimamizi wa maafa nchini.