Habari
Tanzania yakamilisha mfumo wa kurejesha hali baada ya maafa
TANZANIA imekamilisha maandalizi ya Mfumo wa Taifa wa Kurejesha Hali Baada ya Maafa, hatua inayolenga kuimarisha uwezo wa Taifa kukabiliana na athari za majanga yanapotokea.
Mfumo huo unatajwa kuwa sehemu ya mkakati mpana wa Tanzania wa kukabiliana na ongezeko la maafa yanayochangiwa na mabadiliko ya tabianchi, huku ukitoa mwongozo wa hatua za haraka za kurejesha huduma za kijamii, miundombinu muhimu pamoja na shughuli za kiuchumi katika maeneo yaliyoathirika.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya akimwakilisha Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi katika Mkutano wa Sita wa Kawaida wa Kamati ya Mawaziri wenye dhamana ya Usimamizi wa Maafa katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika Mei 11 hadi 14 mjini Masvingo, Zimbabwe.
Alisema mfumo huo umezingatia matumizi ya mifumo ya kisayansi na teknolojia ili kupata taarifa sahihi na za haraka kuhusu madhara ya maafa.
“Mfumo huu utawezesha tathmini ya uharibifu na madhara kwa kutumia mifumo ya kisayansi na teknolojia ili kubainisha kwa haraka hasara katika sekta za uzalishaji wa kiuchumi, miundombinu, huduma za kijamii na sekta mtambuka,” alisema Mhe. Mmuya.
Kwa mujibu wa Mhe.Mmuya, mfumo huo pia umeweka utaratibu wa kuwa na mpango jumuishi wa kurejesha hali katika sekta zilizoathirika huku ukitaka madhara ya maafa kuzingatiwa katika mipango na bajeti za maendeleo za taifa na mamlaka za chini.
Katika hatua nyingine, alisema Tanzania imezindua Mwongozo wa Taifa wa Ugharamiaji wa Maafa wa mwaka 2025 unaolenga kupanua wigo wa upatikanaji wa fedha kwa ajili ya usimamizi wa maafa na shughuli za kurejesha hali kupitia vyanzo vya ndani na nje ya nchi.
“Miongozo hii inaonesha dhamira ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuweka mazingira rafiki ya kisera na kimkakati pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kikanda, kimataifa na sekta binafsi katika usimamizi wa maafa,” alisema
Kwa mujibu wa Mmuya, Tanzania imewekeza katika mifumo himilivu ya chakula na kilimo kutokana na mchango mkubwa wa sekta hiyo katika uchumi wa nchi na ajira kwa wananchi wengi wa ukanda wa kusini mwa Afrika.
Alieleza kuwa kupitia dhana ya Jenga Kesho iliyo Bora (BBT), serikali inaendelea kuwekeza katika matumizi ya teknolojia, taarifa za hali ya hewa, ujenzi wa miundombinu inayozingatia vihatarishi vya majanga pamoja na kuimarisha huduma za kijamii katika maeneo yaliyoathirika.
“Tunaamini ushirikiano wa kikanda na kimataifa ukitekelezwa kwa kuzingatia vipaumbele vya kitaifa utaongeza kasi ya kugeuza hatari za maafa kuwa fursa ya kuimarisha ustahimilivu wa kikanda,” alieleza
Tanzania pia imezialika nchi wanachama wa SADC kutembelea nchini humo kwa ajili ya kubadilishana uzoefu katika maeneo mbalimbali, ikiwemo matumizi ya teknolojia katika usimamizi wa maafa, mifumo ya tahadhari ya mapema, usimamizi wa takwimu pamoja na ujenzi wa Kituo cha Taifa cha Usimamizi wa Maafa kinachotarajiwa kuwa kituo cha umahiri katika ukanda wa SADC mara kitakapokamilika.
=MWISHO=




