Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Taarifa kwa umma uwepo wa Kimbunga “Chido” katika bahari ya Hindi Kaskazini mwa Madagascar


Ofisi ya Waziri Mkuu inatoa taarifa kwa umma kufuatia tahadhari iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuhusu uwepo wa kimbunga “CHIDO” katika Bahari ya Hindi kaskazini mwa kisiwa cha Madagascar. Kimbunga hicho kinatarajiwa kuelekea maeneo ya kaskazini mwa Msumbiji katika kipindi cha siku nne zijazo (tarehe 13 hadi 16 ya mwezi Disemba, 2024).

Aidha, kwa sasa, kimbunga hicho hakiashirii uwezekano wa kusababisha athari za moja kwa moja hapa nchini. Hata hivyo, kutokana na ukaribu wa maeneo ambayo kimbunga “CHIDO” kinatarajiwa kupita (kaskazini mwa Msumbiji) na maeneo ya kusini mwa nchi yetu, upo uwezekano mdogo wa matukio ya vipindi vifupi vya mvua kubwa itakayoambatana na upepo mkali na mawimbi makubwa ya bahari kwa maeneo ya Mtwara na maeneo jirani hususan kati ya tarehe 14 na 16 ya Disemba 2024.

USHAURI: Wananchi wanaoishi kando kando ya bahari, watumiaji wa bahari na wananchi wengine waliopo katika mikoa ya kusini wanashauriwa kuchukua tahadhari na kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania. Vile vile, Mamlaka za Serikali za Mitaa zikiongozwa na Kamati za Usimamizi wa Maafa katika ngazi za mikoa, wilaya, kata na kijiji/mtaa zinatakiwa kuchukua hatua za tahadhari na kusimamia utekelezaji wake kwa wananchi waliopo katika maeneo yao.

Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kufuatilia kwa ukaribu mwenendo wa kimbunga hicho.

(Mwisho)

 

Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu)

12 Disemba,2024