Habari
Simba inaupiga mwingi Kimataifa-Majaliwa
06 Aprili, 2022
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameipongeza timu ya mpira wa miguu ya Simba kwa kuipeperusha vema bendera ya Taifa katika mashindano ya Shirikisho la Klabu Afrika.
“Mwenye macho haambiwi tazama, sote tumeshuhudia wakiendelea kuupiga mwingi na kutuwakilisha vema katika medani za kimataifa. Hakika kwa mpira mzuri wanaocheza wanakonga nyoyo ya mashabiki wa mchezo wa mpira wa miguu nchini.”
Ametoa pongezi hizo leo (Jumatano, Aprili 6, 2022) alipowasilisha hotuba kuhusu Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa Mwaka 2022/2023, Bungeni jijini Dodoma.
“...Nitumie fursa hii kuendelea kusisitiza umuhimu wa michezo kwa kuvipongeza vilabu vyetu vya mpira wa miguu vinavyoshiriki kwenye mashindano ya Ligi Kuu Tanzania Bara (NBC Premier League) na Ligi Kuu Zanzibar (PBZ Premier League).”
Pia, Waziri Mkuu amewapongeza wachezaji mahiri wa vilabu mbalimbali vya mpira wa miguu nchini vikiwemo Yanga - Timu ya Wananchi; Simba - Wekundu wa Msimbazi; Namungo - Wauaji wa Kusini; Azam - Wazee wa Lambalamba.
Vilabu vingine ni Biashara United - Wanajeshi wa Mpakani; Dodoma Jiji - Walima Zabibu; Tanzania Prison – Wajelajela; Mtibwa Sugar - Wakata Miwa na Kagera Sugar – Wanankurukumbi; KMKM, Mlandege, Malindi, Mafunzo na vilabu vinginevyo.
Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imeendelea kufanya jitihada mbalimbali kuhakikisha sekta ya michezo nchini inapiga hatua.
Amesema lengo ni kuimarisha michezo, sanaa na utamaduni ili ziweze kuchangia vema katika Pato la Taifa sambamba na kuzalisha ajira kwa vijana, kutangaza utalii, kuimarisha umoja wa kitaifa na afya za Watanzania.
“Nitumie fursa hii kuwapongeza kwa dhati wanamichezo wote ambao wameiletea heshima nchi yetu kwa kupeperusha bendera nje ya nchi.” Tuna timu za mpira wa miguu, ngumi na wasanii mbalimbali.”
Kwa upande wa mchezo wa ngumi, Waziri Mkuu amewapongeza wanamasumbwi Hassan Mwakinyo, Tonny Rashid, Twaha Kiduku na Ibrahim Class kwa ushindi mnono uliowawezesha kupata mikanda katika mashindano mbalimbali ya kimataifa waliyoshiriki.
“Nitumie fursa hii pia kuzipongeza timu za mpira wa miguu za wanawake kwa ushindi wao katika mashindano mbalimbali ya kimataifa. Kipekee, niwapongeze Timu ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars) kwa kutwaa ubingwa katika mashindano ya COSAFA mwaka 2021.”
Vilevile, Waziri Mkuu ameipongeza Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu ya Watu wenye Ulemavu (Tembo Warriors) kwa kufuzu mashindano ya dunia yatakayofanyika Oktoba, 2022 nchini Uturuki. “Hii ni mara ya kwanza Timu ya Taifa kushinda na kushiriki moja kwa moja mashindano ya dunia.”
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema katika mwaka 2021/2022, Serikali imekamilisha ujenzi wa Mfumo wa Usajili na Usimamizi wa Wasanii na Wadau wa Sanaa na kuboresha mfumo wa usajili kwa njia ya kielektroniki.
Amesema mfumo huo, umewezesha wabunifu 485 na kazi zao 2,921 kusajiliwa, na Serikali imewezesha wasanii wa fani ya muziki ambao kazi zao zimetumika kwenye vituo vya redio na televisheni kupata mirabaha. “Nitoe wito kwa wasanii wote nchini kujisajili katika mfumo huo ili kupata manufaa tarajiwa.”
Pia, Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuliomba Bunge liidhinishe shilingi bilioni 148.89. Kati ya fedha hizo shilingi bilioni 101.36 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 47.52 ni kwa ajili matumizi ya maendeleo.
Vilevile, Waziri Mkuu ameliomba Bunge liidhinishe shilingi bilioni 132.72 kwa ajili ya Mfuko wa Bunge. Kati ya fedha hizo shilingi bilioni 127,32 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 5.40 ni kwa ajili matumizi ya maendeleo.