Habari
Serikali yaweka mkazo ushiriki sawa wa jinsia Baraza la Vyama vya Siasa
Serikali yaendelea kuhimiza ushirikishwaji sawa wa kijinsia katika Baraza la Vyama vya Siasa ili kuendelea kutimiza wajibu wake wa kikatiba na kisheria katika kulijenga taifa.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu ( Sera Bunge na Uratibu na Wenye Ulemavu) Prof. Palamagamba Kabudi katika tukio la uzinduzi uongozi mpya wa Baraza la Vyama vya Siasa na Nembo ya Baraza la Siasa lililofanyika Jijini Dar es Salaam.
Waziri Kabudi amemshukuru Mhe. Rais, Dkt, Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuvipa nafasi sawa vyama vya siasa ya kukutana naye, kujadiliana na kutoa maoni yao.
“Vikao vya Baraza la Vyama vya Siasa ni muhimu katika kuongeza uelewa umuhimu mfumo wa demokrasia ya vyama vingi, ambao sio vitisho au uhasama ni mfumo wa kuwasaidia wananchi wenye mawazo tofauti na maoni tafauti kukaa pamoja kujadili mstakabili wa taifa lao, “ alieleza.
Aidha uzinduzi wa nembo ya baraza itatumika kutambulisha baraza lakini nembo hiyo itakuwa ni alama katika matumizi ya nyaraka za Baraza la Vyama vya Siasa.
kwa upande wake Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji Fransis Mutungi alisema nchi yetu ni mfano wa kuigwa kwa utamaduni uliojengwa wakukaa pamoja licha ya tofauti ya kisiasa jambo hilo ni tunuu ambayo inapaswa kulindwa.
"Alisema hata inapotokea ukinzani wa hoja, huwa tunaibuka na hoja za kitaifa, hivyo tunapaswa kuendelea kulijenga baraza hili liwe mfano wa kuingwa katika bara la afrika," alieleza Msajili
Ofisi ya Msajili itaendelea kuhakikisha kwamba Baraza la Vyama vya Siasa linaendelea kuwa jukwaa imara la majadiliano ushauri na ushirikiano katika kukuza na kudumisha siasa za kistaarabu.
Awali Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa Ndg. Aggrey Mwanri alisema baraza hili halimnyimi mtu kuwa na mawazo mbadala, lakini tunajadiliana hoja zenye maslahi mapana ya ustawi wa nchi yetu kwa kuangalia mshikamano wa nchi, na umoja wa taifa letu.
Naye Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Wakili Boniface Mwabukusi, alitoa rai kwa kwa msajili wa vyama vya siasa kupitia sheria ya vyama vya siasa kuona umuhimu wa kuanzishwa kwa kamati ya siasa kushughulikia makosa ya kisiasa ili kutatua changamoto za kisiasa kabla ya kupelekwa katika mifumo mingine.




