Habari
Serikali kuja na maelekezo kuimarisha utendaji kazi Ofisi za Konga
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene amesema serikali itatoa maelekezo kwa Halmashauri kuweka mipango maalumu ya kuziwezesha ofisi za vikundi vya watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI (Konga) katika maeneo ya usimamizi, ruzuku na mikopo. Ili kuwa imara na endelevu na kuwa na mchango mkubwa katika kufikia malengo ya kitaifa na dunia kuhusu UKIMWI.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene wakati wa uzinduzi wa magari nane ya mradi wa HEBU TUYAJENGE uliofanyika katika Ofisi za NACOPHA Mbezi Beach Dar es salaam.
“Serikali inatambua umuhimu wa mifumo ya kijamii kwa sababu ina mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa. Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Tume ya Kudhibiti UKIMWI itaendelea kuhakikisha Uratibu wa Sera na miongozo unatoa fursa ya kuziwezesha Konga za WAVIU”
Aidha, katika hotuba yake, Mheshimiwa Rais alitoa maelekezo mahususi kwa Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia TACAID, Wizara ya Afya na wadau wengine kuweka jitihada na mikakati madhubuti katika kuzuia maambukizi mapya ili tuweze kufikia hatua ya kutokomeza kabisa.
Ikiwa ni pamoja na Kuimarisha huduma za upimaji wa VVU na matumizi ya ARV ili kutokomeza vifo vitokanavyo na UKIMWI, kuweka mikakati ya kutokomeza ubaguzi na unyanyapaa kwa WAVIU.
“Ofisi ya Waziri Mkuu chini ya Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itayatekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais kwa haraka ikiwa ni pamoja na kuziratibu Wizara husika na Wadau katika kuhakikisha maelekezo haya yanatekelezwa kwa wakati, alisema Waziri.”
Naye Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Bwn. Kaspar Mmuya amewapongeza NACOPHA kwa kazi nzuri ya kupambana na maambukizi ya virusi vya UKIMWI.
“Kuhamasisha watu kujitokeza na kupima afya zao ni njia mojawapo ya kukabiliana na maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI.”
Akitoa taarifa Mwenyekiti wa Baraza la Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (NACOPHA) Bi, Leticia Mourice Kapela, amesema baraza limeneemeka kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu kwa upande wa vijana, wanawake na WAVIU kwa ujumla.
“Uwezeshi huu katika fursa za mafunzo, mitaji ya kifedha, vifaa vya kuanzia shughuli za ujasiriamali, umesaidia vijana WAVIU kupata ujasiri wa kukabiliana na kuziepuka changamoto mbalimbali zinazowaweka katika hatari ya kupata maambukizi, ikiwemo kuanza ngono katika umri mdogo, kuwa na mahusiano na watu wenye umri mkubwa na ulevi wa kupindukia”
Naye Mkurugenzi TACAIDS Bi. Audrey Njelekela, amesema Konga ziko kwenye Halmashauri 184 na Afua zote zinatekelezwa kwa kushirikiana na Halmashauri.
“Kupata magari kutasaidia kuongeza kasi na ufanisi katika kuhakikisha muitikio wa kitaifa unatekelezwa”