Habari
Serikali imeanza kufanyia kazi taarifa ya CAG-Waziri Mkuu
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali tayari imeanza kuifanyia kazi taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya mwaka baada ya kuwasilishwa rasmi Bungeni Aprili 6, mwaka huu.
“Tarehe 6 Aprili 2023, Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali iliwasilishwa hapa Bungeni ikiwa ni utekelezaji wa takwa la kikatiba linaloielekeza Serikali kuwasilisha Bungeni taarifa hiyo ndani ya siku saba za kazi kuanzia siku ya kikao cha kwanza cha Bunge tangu ilipowasilishwa kwa Mheshimiwa Rais. Nitumie fursa hii kuliarifu Bunge lako tukufu kwamba, baada ya ripoti hiyo kuwasilishwa Bungeni, tayari Serikali kwa upande wake imeanza kuifanyia kazi mara moja,” amesema.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Aprili 13, 2023) wakati akihitimisha hoja zilizotolewa na Wabunge wakati wakijadili Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2023/2024.
Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa anatambua hisia za Waheshimiwa Wabunge pamoja na wananchi kwa ujumla kuhusu ubadhirifu wa mali na fedha za umma uliobainishwa kwenye taarifa hiyo. “Sote tulishuhudia namna Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alivyoonesha kutoridhishwa na ubadhirifu uliobainishwa katika taarifa hiyo.”
Amelieleza Bunge kuwa miongoni mwa hatua zinazochukuliwa na Serikali ni kuhakikisha Maafisa Masuuli wote wanaandaa majibu ya hoja, kama inavyoelekezwa katika sheria na kanuni za ukaguzi wa umma.
“Nitumie fursa hii, kuwakumbusha Maafisa Masuhuli wote wazingatie maelekezo ya Mheshimiwa Rais ya kuhakikisha wanapitia kwa kina taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kujibu na kuchukua hatua za haraka juu ya hoja zote zilizoibuliwa kwenye maeneo yao,” amesisitiza.
Waziri Mkuu amesema pamoja na hatua zinazochukuliwa na Serikali, taarifa ya kina kwenye maeneo yaliyobainishwa katika ripoti ya CAG, itawasilishwa Bungeni kwa kuzingatia kanuni husika.
“Nilihakikishie Bunge na wananchi kuwa kwa kuzingatia msimamo wa Mheshimiwa Rais, Serikali ya awamu ya sita haitafumbia macho matumizi mabaya ya rasilimali za umma na kuwa hatua zinazochukuliwa na zitakazochukuliwa zitakuwa endelevu.”
Bunge limeidhinisha bajeti ya sh. 339,361,007,000 ambapo sh. 173,733,110,000 ni kwa ajili ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake na sh. 165,627,897,000 ni kwa ajili ya Mfuko wa Bunge.
Akiwasilisha makadirio na matumizi ya ofisi yake Aprili 5, mwaka huu, Waziri Mkuu aliliomba Bunge liiidhinishe sh. 173,733,110,000/- ambapo kati ya fedha hizo, sh. 121,364,753,320/- ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh. 52,368,356,680/- ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo kwa Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake.
Vilevile, aliliomba Bunge liidhinishe jumla ya sh. 165,627,897,000/- kwa ajili ya Mfuko wa Bunge ambapo sh. 160,458,877,000/- ni za matumizi ya kawaida na sh. 5,169,020,000/- ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.