Habari
Rais Samia kuongoza maziko ya Hayati Lowassa Februari 17, 2024
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuongoza maziko ya Waziri Mkuu mstaafu Hayati Edward Lowassa yatakayofanyika katika Kijiji cha Ngarash Halmashuri ya Wilaya ya Monduli Mkoani Arusha tarehe 17 Februari, 2024.
Mhe. Jenista ameyasema hayo wakati wa mahojiano maalum na waandishi wa habari kijijini cha Ngarash ambapo amesema maandalizi ya kuhifadhi mwili wa Hayati Edward Lowassa yamekamilika ambapo viongozi mbalimbali wa Kitaifa kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Tanzania Bara wanatajarajiwa kushiriki maziko hao.
Amesema maziko hayo yataambatana na Gwaride maalum la mazishi ya viongozi Kitaifa ambalo tayari limekwishaandaliwa.
“Tunamshukuru Mwenyezi Mungu taratibu zote zimekamilika nyumba yake ya milele (kaburi) la kumhifadhi liko tayari, parade la mazishi ya viongozi Kitaifa liko tayari pamoja na huduma nyingine kama maandalizi ya ibada na tunatarajia viongozi wetu wa Kitaifa watakaojumuika na sisi wakiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. na Amiri Jeshi Mkuu Samia Suluhu Hassan,”Amesema Mhe. Jenista.
Pia ameendelea kutoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na watanzania kwa ujumla kufuatia msiba huo wa kiongozi muhimu kwa Taifa akisema utendaji wake mwema kwa Tiafa utaendelea kukumbukwa kwa moyo wake wa uzalendo aliuonesha kuhakikisha watanzania wanapata maendeleo kupitia nafasi zote alizowahi kuzitumikia enzi za uhai wake.
“Kwa niaba ya Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali tunaendelea kutoa pole sana kwa familia na mjane mke wa Hayati Edward Lowassa Mama Regina Lowassa, watoto, ndugu, rafiki na jamaa tutaendelea kuenzi na kuyakumbuka mema yote aliyoyatenda akiwa kiongozi mwandamizi ndani ya Serikali na Sekta mbalimbali alizowahi kufanya kazi,”Ameeleza .
Aidha Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu)Dkt. Jim Yonazi amebainisha kwamba Serikali imeshirikina na sekta mbalimbali katika masuala ya ulinzi na usalama, usafirishaji wa waombolezaji na kuhakikisha maandalizi yote yakamilika kwa wakati huku akiwashukuru wakazi wa Monduli na mkoa wa Arusha kwa upendo wao waliouonesha pamoja na viongozi wa dini.
“Niwahakikishie kwamba uratibu wa jambo hili umekamilika eneo la maziko limekamilika na itifaki zote za kiserikali na kimila zimekamilika nitumie nafasi hii kuwashukuru wakazi wa Arusha kwa moyo wao wa upendo na viongozi wa dini kuwa sisi wakati wote. Serikali iko tayari kuendelea kushirikiana nao na tuaamini shughuli hi itafanyika kwa wema ili kumhifadhi kiongozi wetu,”Amesema Dkt. Yonazi.
Ikumbukwe Waziri Mkuu mstaafu Hayati Edward Lowassa alizaliwa Agosti 26, 1953 na kufariki dunia tarehe 10 Februari , 2024 wakati akipatiwa matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Jijini Dar es Salaam.
=MWISHO=