Habari
Mhe.Nderiananga agawa futari kwa Watu Wenye Ulemavu Zanzibar
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mheshimiwa Ummy Nderiananga amegawa futari kwa watu wenye ulemavu 500 kutoka Wilaya Saba za Mkoa wa Kusini Unguja.
Akizungumza katika ukumbi wa Dkt. Ali Mohamed Shein, Tunguu, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar Mhe. Nderiananga aliwaomba waumini wa dini ya kiislamu na watanzania wote kuutumia mwezi Mtukufu wa Ramadhan kwa kufanya ukarimu kwa wanyonge, wasiyojiweza na watu wenye ulemavu.
Mhe. Nderiananga amegawa futari hiyo kwa kushirikiana na Shirika lisilo la kiserikali linaloshughulikia watu wenye ulemavu la Tanzania Foundation for Excellence in Disabilities (TFED) iliyoambatana na dua maalum ya kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi katika utekelezaji wa majukumu yao ili Taifa liwe na amani, umoja na mshikamano.
“Nimshukuru sana Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani viongozi wetu hawa wamekuwa watu wema wametujali na kututhamini wakati wote. Sisi watu wenye ulemavu Watoto wa Dkt. Samia na Dkt. Mwinyi tumeona ushirikishwaji mkubwa katika serikali na sekta binafsi,” Mhe. Nderiananga.
Pia alimpongeza Dkt. Samia kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati kwani ni nia yake njema kwa watanzania wote kuwa na maendeleo huanzia ngazi ya familia hadi Taifa kwa ujumla.
Vilevile alitumia nafasi hiyo kumpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kazi kubwa aliyoifanya katika utekelezaji wa miradi ya kimaendeleo kama ujenzi wa Barabara kwa kiwango cha lami.
“Mheshimiwa Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi amefanya kazi kubwa sana hapa Zanzibar barabara zimejengwa kila mahali watu wanaendelea na shughuli zao. Sekta ya afya Dkt. Mwinyi amewashangaza wengi kwa ujenzi wa hospitali za Wilaya zenye vifaa tiba vya kisasa, sekta ya maji na elimu ambapo tunashuhudia ujenzi wa shule katika maeneo yetu,”Alipongeza.
Aidha aliwasisitiza wazazi na walezi kutowaficha watoto wenye ulemavu ndani na badala yake wawapeleke shule kwani Serikali iko tayari kwa ajili ya kuwahudumia kuhakikisha wanatimiza ndoto zao na kuwa nguvu kazi ya Taifa.
Kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani inayotarajiwa kuadhimishwa Machi 08 mwaka huu ameiomba jamii kuendelea kuiamini nafasi ya mwanamke katika uongozi akisema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni mfano wa kuigwa hivyo wanawake hawana budi kujitokeza kugombea katika nafasi mbalimbali pindi wakati utakapowadia wa uchaguzi unatakaofanyika mwezi Oktoba 2025.