Habari
Naibu Waziri Ummy awataka Watu wenye Ulemavu kuchangamkia fursa Mikopo inayotolewa na Halmashauri
NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika na Watu wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga amewataka wenye Ulemavu nchini kutumia fursa ya mikopo ya asilimia 2 inayotolewa na Halmashauri kujiinua kiuchumi.
Naibu Waziri Ummy alitoa kauli hiyo Oktoba 22, 2021 alipotembelea wilaya ya Same, Mwanga na Moshi mkoani Kilimanjaro na kuzungumza na watu wenye ulemavu ambapo alisema kuwa, Serikali kupitia uongozi mahiri wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuwajali watu wenye ulemavu kwa kupunguza masharti ya ukopaji wa mikopo hiyo ambapo awali ilikuwa ikitolewa kwa kikundi lakini kwa sasa anakopeshwa hata mmoja.
“Katika fedha ambazo serikali imetenga kwa kila halmashauri nchini asilimia mbili ya mapato ya ndani imetegwa kwa ajili ya kuwakopesha Watu wenye Ulemavu, hivyo tunawajibu wa kuchangamkia fedha hizo na kuzitumikia katika kukuza uchumi wetu” alisema Naibu Waziri Ummy.
Alisema kuwa, zipo baadhi ya halmashauri nchini Watu wenye Ulemavu wamekuwa na muamko kidogo katika kuchangamikia fursa hiyo ikiwemo wilaya ya Mwanga na kutoa wito kwa maafisa ustawi wa jamii na maafisa maendeleo kuendelea kuhamasisha ili wajitokeze kwa wingi. Aliongeza kuwa, Watu wenye Ulemavu wamekuwa wakichukua mikopo ya halmashauri na kurejesha kwa wakati.
Sambamba na hayo Naibu Waziri Ummy alisema kuwa, Watu wenye Ulemavu wanauwezo mkubwa wa kufanya kazi ambapo alikipongeza kikundi cha watu wenye ulemavu cha Thunga group kwa jinsi walivyotumia mkopo walioupata halmashauri kuanzisha duka la rejareja na wakala wa kutoa hela kwenye simu.
“Watu wenye Ulemavu hatupaswi kukata tamaa pindi tunapozarauli na wala tusibweteke wala kuvunjika moyo kwani viongozi wapo mstari wa mbele kututetea na kutuunga mkono” alisema Naibu Waziri Ummy.
Naibu Waziri Ummy alisema kuwa, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ametenga Bilioni 4 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni 50 ya wanafunzi wenye Ulemavu ambapo kwa mkoa wa Kilimanjaro umepata mabweni mawili yatakayojengwa wilaya ya Mwanga na Moshi.
“Watu wenye ulemavu tunamshukuru sana Rais Samia kwa jinsi ambavyo anatujali na mara nyingi ameonyesha kutufariji na kutufanya na sisi tujione ni sehemu muhimu kwake na katika serikali” alisema.
Naibu Waziri huyo alitumia nafasi hiyo kuziomba halmashauri zilizopata fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabweni kuhakikisha wanazingatia mahitaji ya walemavu katika ujenzi wake pamoja na kusimamia fedha hizo ili thamani ya majengo iendane na thamani ya fedha.
Akisoma taarifa ya mikopo ya Watu wenye Ulemavu katika wilaya ya Same, Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Anastazia Tutuba alisema kuwa katika mwaka wa fedha 2020/2021 halmashauri hiyo ilitoa mikopo jumla ya Tsh milioni 229 katika vikundi vya Vijina, Wanawake na Wenye Ulemavu. Aidha Mkurugenzi huo alieleza kuwa, jumla ya vikundi 10 vya Watu wenye Ulemavu vilipewa mikopo yenye thamani ya milioni 35.8.
Kw upande wake, Mwenyekiti wa halmashauri ya Mwanga, Salehe Mkwizu alitumia nafasi hiyo kuiomba Serikali kujenga chuo cha ufundi stadi kwa ajili ya Watu wenye Ulemavu ili kuwasaidia kuwajengea uwezo wa kukuza vipaji walivyonavyo.