Habari
Naibu Waziri Nderiananga Akutana na UNICEF kujadili mikakati ya kuwalinda watoto wenye ulemavu dhidi ya madhara ya EL NIÑO.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga pamoja na wataalam kutoka Idara ya Menejimenti ya Maafa na Kitengo cha Huduma kwa Watu Wenye Ulemavu amekutana na Ujumbe kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) kwa lengo la kujadili mikakati ya kuwasaidia watoto wenye ulemavu katika kujiandaa, kukabiliana na kurejesha hali baada ya madhara yanayoweza kusababishwa na mvua za El Niño, Kikao hicho kimefanyika Oktoba 9, 2026 katika Ofisi ya Waziri Mkuu jijini Dodoma.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho Naibu Nderiananga, ameipongeza UNICEF kwa utayari wake wa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuimarisha ulinzi na usalama wa watoto wenye ulemavu wakati wa maafa, Amesisitiza umuhimu wa kundi hilo kupewa kipaumbele kutokana na changamoto zinazoweza kukabili katika hatua za tahadhari, uokoaji na urejeshaji wa hali baada ya maafa.
Mhe. Nderiananga amesema, Sheria ya Maafa imeweka msingi wa kugawa majukumu ya usimamizi na kukabiliana na maafa kuanzia ngazi ya Taifa hadi kata,aidha amewahimiza UNICEF na wadau wengine kushirikiana na Serikali katika upatikanaji wa vifaa vya uokoaji na urejeshaji wa hali, pamoja na kuunga mkono juhudi zinazotekelezwa kupitia Mfuko wa Taifa wa Maafa.
Katika kuimarisha upatikanaji wa taarifa za tahadhari kwa watu wenye ulemavu, Ofisi ya Waziri Mkuu imeandaa vipeperushi vya Nukta Nundu, maandishi makubwa na video fupi ya Lugha ya Alama, hatua hiyo inalenga kuhakikisha taarifa kuhusu hatua za kuchukua kukabiliana na madhara ya El Niño zinawafikia watu wenye ulemavu kwa njia zinazozingatia mahitaji yao.
Kwa upande wake, Naibu Mwakilishi wa Miradi wa UNICEF Bi. Patricia Lombo, ameipongeza Serikali kwa ushirikiano unaotolewa katika kuboresha ustawi wa watoto, hususani wenye ulemavu.
Amesema, UNICEF iko tayari kuendelea kuiunga mkono Serikali kwa rasilimali fedha na utaalamu katika kuimarisha maandalizi, mwitikio na urejeshaji wa hali baada ya majanga, kwa kuzingatia mahitaji ya watoto wenye ulemavu.




