Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Miradi ya Shilingi Trilioni 18.58 yasajiliwa nchini.


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imefanikiwa kusajili jumla ya miradi ya uwekezaji 294 yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 8.04 ambazo ni sawa na sh. trilioni 18.58 ikilinganishwa na dola za Marekani bilioni moja mwaka 2020/2021.

“Mafanikio hayo yanatokana na ziara mbalimbali za viongozi wa Serikali akiwemo Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alizozifanya nje kwa lengo la kuifungua nchi. Miradi hiyo inatarajiwa kuzalisha ajira takriban 62,301,” amesema. 

Ameyasema hayo leo (Jumatano, Aprili 6, 2022) wakati akiwasilisha hotuba kuhusu Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa Mwaka 2022/2023, Bungeni jijini Dodoma.

Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kutekeleza mikakati ya kuvutia na kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo nchini. “Mikakati hiyo ni pamoja na kuhamasisha ushiriki wa sekta binafsi katika uwekezaji,  kufanya mapitio ya sera, sheria na kanuni zinazosimamia uwekezaji pamoja na kutenga hekta milioni 1.6 za ardhi kwa ajili ya uwekezaji. 

Mheshimiwa Majaliwa amesema katika mwaka 2022/2023, Serikali itaendelea kufanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Uwekezaji ya Mwaka 1996 ili iendane na mazingira ya sasa ya uwekezaji ikiwa ni pamoja na kujumuisha vipaumbele vilivyoainishwa katika Mipango ya Maendeleo ya Taifa. 

Amesema Serikali itaendelea kutekeleza Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Kufanya Biashara nchini ikiwa ni pamoja na kuendelea kuondoa muingiliano wa majukumu kwa taasisi za udhibiti, kuondoa tozo sumbufu na kuimarisha ushirikiano wa sekta ya umma na sekta binafsi. “Aidha, itaimarisha majadiliano na utatuzi wa changamoto zinazoikabili sekta binafsi.”

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema idadi ya watalii walioingia nchini iliongezeka kwa asilimia 48.6 kutoka watalii 620,867 mwaka 2020 hadi watalii 922,692 mwaka 2021. 

Waziri Mkuu amesema utalii wa ndani pia umeendelea kuimarika ambapo idadi ya watalii wa ndani waliotembelea maeneo ya hifadhi iliongezeka kutoka 562,549 mwaka 2020 hadi 788,933 mwaka 2021 sawa na ongezeko la asilimia 40.2. 

Amesema Serikali imeongeza kasi ya utangazaji utalii kitaifa na kimataifa, kuboresha ulinzi na usalama wa rasilimali za maliasili na malikale na kushirikisha jamii katika kutekeleza mipango ya uhifadhi wa ikolojia.

Pia, Mheshimiwa Majaliwa amesema hatua zinazochukuliwa na Serikali zimekuwa chachu ya kuongezeka kwa mapato yatokanayo na watalii wa kimataifa kutoka Dola za Marekani milioni 714.59 mwaka 2020 hadi Dola za Marekani bilioni 1.25 mwaka 2021 sawa na ongezeko la asilimia 76.

Amesema kuimarika huko kwa sekta ya utalii nchini kumetokana na mwelekeo na jitihada za Mheshimiwa Rais Samia katika kuanzisha na kutekeleza Mpango wa Kitaifa wa kukabiliana na janga la UVIKO-19 hapa nchini. 

“Hii ni pamoja na kutekeleza mkakati wa kuinua sekta ya utalii nchini na kutekeleza mpango wa chanjo ya UVIKO-19 kitaifa. Mpango huo wa kitaifa umeleta taswira mpya kiutalii ambapo Tanzania imekuwa eneo salama zaidi kutembelewa na watalii.”

Mheshimiwa Majaliwa amesema pamoja na utekelezaji wa mipango hiyo, kumekuwa na jitihada mahsusi za Mheshimiwa Rais Samia katika kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia programu maalum ya Royal Tour.

Amesema kupitia programu hiyo ambayo itaanza kurushwa kwenye vituo vya runinga hivi karibuni, mtandao maarufu wa habari nchini Marekani wa theGrio umetambua juhudi za Mheshimiwa Rais Samia katika kuiongoza vema sekta ya utalii nchini na kuifanya Tanzania kuwa kivutio cha kwanza cha utalii Afrika mwaka 2022. 

Pia, Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuliomba Bunge liidhinishe jumla ya shilingi bilioni 148.89 kwa ajili ya Ofisi ya Waziri Mkuu ambapo kati ya fedha hizo shilingi bilioni 101.36 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 47.52 ni kwa ajili matumizi ya maendeleo.

Vilevile, Waziri Mkuu ameliomba Bunge kuidhinisha shilingi bilioni 132.72 kwa ajili ya Mfuko wa Bunge. Kati ya fedha hizo shilingi bilioni 127.32  ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 5.40 ni kwa ajili matumizi ya maendeleo.

-End-