Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Miaka 60 ya Muungano Tanzania yapata Rais wa kwanza mwanamke: Waziri Mhagama


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Mheshimiwa Jenista Mhagama amesema kuwa katika maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano kwa mara ya kwanza Tanzania inajivunia kuwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa kwanza mwanamke ambaye ni Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Ameyasema hayo leo Aprili 8, 2024 jijini Dodoma wakati wa hafla ya uzinduzi wa nembo na kauli mbiu ya miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Tunapofikia maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano wa Tanzania tunaongozwa na Rais mwanamke mbobezi Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na nchi yetu imeweza kupata mafanikio makubwa katika pande zote mbili za Muungano. Hili ni jambo la kujivunia ni Rais mbunifu, mwenye uwezo wa hali ya juu na aliyethibitisha ndani na nje ya nchi juu ya utendaji wake wa kazi uliotukuka”.alisema Mhe. Mhagama

Aidha, Mheshimiwa Waziri Jenista amesema kuwa mwaka 2024, Watanzania wanajivunia kwa kutimiza miaka 60 ya Muungano  kwa sababu nyingi za kihistoria, kijiografia, kitamaduni, kibiashara, kisiasa na kiusalama ambazo wakati wote wa Muungano zimeendelea kuwaunganisha kama Taifa moja la Tanzania.

“Sote tunafahamu uzito wa maadhimisho ya miaka 60 ya tukio lolote lile. Hii ni Jubelei ya almasi. Hivyo, hatuna budi kukaa pamoja kama Taifa moja kumshukuru Mungu na kuiadhimisha kwa furaha kubwa”, amesisitiza Waziri Mhagama.

Sambamba na uzinduzi wa miradi ya maendeleo, wakati wa maadhimisho hayo Mheshimiwa Jenista ametaja matukio mengine yatakayoambatana na maadhimisho hayo kuwa ni  uzinduzi wa Kitabu cha Historia ya Muungano Aprili 23, 2024 katika Kituo cha Mikutano cha Mwalimu Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.

Pamoja na tukio la kutunuku nishani za heshima kwa viongozi mbalimbali Serikalini na Jeshini pamoja na askari kwa kutambua mchango wao katika kudumisha Muungano ambapo nishani hizo zitatunukiwa na Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan Aprili 24, 2024 katika viwanja vya Ikulu, jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mheshimiwa Dkt. Selemani Jafo amesema “Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa Mheshimiwa Rais Samia kwa kushirikiana na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Wawakilishi, Dkt. Hussein Mwinyi imeweza kutatua hoja 15 za Muungano kati ya 18 katika kipindi cha miaka mitatu”.

Naye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Mheshimiwa Hamza Hassan Juma amewataka Watanzania kuendelea kudumisha Muungano kutoka na kuwa tuni hiyo iliyowekwa na waasisi wa Muungano Hayati Julius Kambarage Nyerere na Abeid Aman Karume.

“Miaka 60 ya kuungana kwetu ni jambo la kujivunia kwa Watanzania hadi sasa chini ya uongozi wa Rais Samia na Dkt. Hussein Mwinyi wameendelea kuimarisha Muungano wetu”, ameeleza Mheshimiwa Hamza

Sherehe za kilele cha Maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano zitazinduliwa rasmi na Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi tarehe 14 Aprili, 2024 katika Uwanja wa Maisara, Zanzibar. Ambapo tukio hilo litafuatiwa na uzinduzi wa miradi ya maendeleo katika maeneo mbalimbali nchini.

Aidha, Kilele cha sherehe za maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano zitafanyika   Aprili 26, 2024 katika Uwanja wa Uhuru – Dar es Salaam ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amir Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwaongoza Watanzania wote katika kusherehekea maadhimisho hayo.

=Mwisho=