Habari
Mhe. Hemed Suleiman: “Tanzania kufanya Sensa ya aina yake”
Makamu wa Pili wa Rais, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdullah ameeleza kuwa Nchi ya Tanzania imejipanga kufanya ya sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 kwa njia ya kidijitali ambapo itarahisisha ukusanyaji wa taarifa wakati wa zoezi hilo.
Ametoa kauli hii wakati akifunga mafunzo ya Wakufunzi wa sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 ngazi ya Taifa uliofanyika katika Ukumbi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa Mkoani Iringa tarehe 01 Julai, 2022.
Makamu wa Pili wa Rais alisema kuwa, sensa ya mwaka huu itaendeshwa kwa mifumo ya kitehama ambapo itakuwa ni mara ya kwanza kwa nchi kuwa na mfumo mpya utakaongeza ufanisi.
“Sensa ya mwaka huu ni ya sita itakayobebwa na upekee wa aina yake kwani inaunganisha matukio mawili makubwa ya kitaifa ikiwemo la ukusanyaji wa taarifa za majengo yote nchini pamoja na taarifa za idadi ya watu,” alieleza.
Aidha alisema hadi sasa maandalizi yake yamefiki asilimia 87 na hii inaonesha ni hatua nzuri kwa taifa hivyo watu waendelee kupewa elimu kwa wingi.
“Kuhesabu watu kitaalam itasaidia kupata taarifa kwa urahisi, na kazi hii itafanyika kwa umakini mkubwa hivyo tuifanye kwa weledi na viwango vinavyotakiwa,”aliongezea Mhe. Abdallah
Sambamba na hilo alitoa rai kwa wakufunzi hao kuendelea kuzingatia uzalendo katika utekelezaji wa majukumu yao.
“Wahitimu wetu wote zingatieni uzalendo na muwe vielelezo vizuri kwa kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha wananchi kujitokeza katika zoezi hili la sensa ili kuleta matokeo makubwa,”alisisitiza.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene alieleza kuhusu utekelezaji wa zoezi la Operesheni Anwani za Makazi kuwa umefikia asilimia 95, hii ikiwa ni muunganiko wa utekelezaji wa shughuli zote zilizopangwa.
Aidha alisema kuwa, Kazi zinazoendelea kufanyika kwa sasa ni kuhakiki na kusafisha taarifa za anwani pamoja na kuweka miundombinu ya anwani za makazi inayojumuisha nguzo za majina ya barabara na kubandika vibao vya namba za nyumba/anwani kwenye majengo.
“ Licha ya kuwa hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa Operesheni hii kuwezesha zoezi la Sensa kufanyika kwa tija, Operesheni hii imeacha alama katika kuimarisha ustawi wa jamii, Vijiji na Miji, Mamlaka za Serikali za Mitaa, Mikoa na Taifa katika nyanja mbalimbali ikiwemo Uchumi wa Kidijitali,”alisema Mhe. Simbachawene
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Hamad Hassan Chande alisema kuwa, zoezi la sensa ya watu na makazi ni nyenzo muhimuu kwa kuzingati tija iliyopo hususan katika masuala ya mipango ya maendeleo ya nchi yetu kwa kuzingatia uwepo wa bajeti yenye kukidhi mahitaji yaliyopo.
“Matokeo ya sensa ya mwaka 2022 yatatoa mwelekeo mzima wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe Samia Suluhu Hassan kuhusu utekelezaji wa ahadi zilizotolewa kwa wananchi wetu kupitia ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020-2025, na matokeo haya ni nyenzo muhimu kwa wizara yangu kwani yatasaidia kufuatilia utekelezeaji wa bajeti katika sekta zote,”alisisitiza.
AWALI
Wakufunzi zaidi ya 500 wamehitimu mafunzo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 kwa ngazi ya Taifa yaliyofanyika katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa Mkoani Iringa tarehe 01 Julai, 2022 ambapo wakufunzi hao walitumia jumla ya siku 21 kupatiwa ujuzi huo.
=MWSIHO=