Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Meja Jenerali Mumanga “Mpango wa Taifa wa Kujiandaa na Kukabiliana na Maafa Kupunguza Vihatarishi vya maafa”


Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeanzisha Mpango wa Taifa ya Kujiandaa na kukabiliana na Maafa pamoja na Mkakati wa Mawasiliano wa Dharura unaolenga kupunguza vihatarishi vya maafa ili kuepusha madhara yatokanayo na maafa nchini.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Meja Jenerali Michael Mumanga wakati akiwasilisha hotuba kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu wakati wa ufunguzi wa Jukwaa la Taifa la Wadau wa Udhibiti wa maafa kwa ajili ya kuthibitisha Mpango huo lililofanyika Mount Meru hotel Mkoani Arusha lililokutanisha wadau kutoka Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Kimataifa, Asasi za Kiraia na wawakilishi wa Wizara, Idara na Taasisi za Serikali.

Meja Jenerali alieleza kuwa, kutokana na uwepo wa athari za maafa katika jamii Serikali kwa kushirikiana na wadau imeona ni muhimu kuwa na mipango na mikakati madhubuti yenye lengo la kujiandaa na kupunguza vihatarishi vya maafa kwa kadiri inavyowezekana ili kujenga jamii iliyo na ustahimilivu.

"Tunaamini jitihada za pamoja na wadau zitasaidia katika kukabili majanga nchini kwani kumekuwa na matukio ya majanga ambayo yamekuwa yakisababisha maafa na kuathiri mfumo wa kawaida wa maisha katika jamii kupelekea matokeo hasi katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi kutokana na kupotea kwa mafanikio yaliyopatikana kwa muda mrefu na hivyo kuzorotesha hatua za maendeleo zilizokwishafikiwa katika maeneo husika hivyo”,alieleza Meja Jenerali Mumanga.

Aidha alisema majanga yapo mengi ya asili na yatokanayo na shughuli za kibinadamu hivyo ipo haja ya kila mmoja wetu kwa kushirikiana na wadau kufanya kazi kwa ufanisi kuhakikisha tunasaidia jitihada hizi za kukabiliana na maafa.

“Maafa yapo kila sehemu yanatofautiana kwa vyanzo vyake, hivyo mpango huu umekuwepo tangu 2012 ni kweli kwamba ipo haja ya kuuhuisha kwa kuzingatia muda na matukio yanabadilika, hivyo kuhuishwa kwa mpango huu kutaendana na hali halisi ya sasa ya kukabiliana na maafa nchini,”alisisitiza.

Kwa upande wake Mkuu wa uendeshaji UNDP Bw. Bwana Jeremiah Mallongo akiwaslilisha hotuba kwa niaba ya Mratibu mkazi wa shirika hilo alisema jukwaa hilo limewakutanisha kwa siku tatu na kueleza litasaidia kuhuisha mpango ili kuwa na uhalisia katika kukabili maafa, hivyo lengo ni kuendelea kupunguza vihatarishi vya maafa na athari zake.

“UNDP tunafuraha kuratibu jukwaa hili kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu kuhakikisha tunaendelea kuweka mikakati ya kupunguza athari za majanga nchini kwani majanga yatakuwepo kutokana na sababu mbalimbali ila lengo kuu ni kuweza kuyakabilia na kupunguza athari zake,”alisema Mallongo

Naye Naibu Kamishna Operesheni kutoka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Bw.Charo Mangale amewasihi wananchi kuendelea kutoa taarifa za majanga mapema kunusuru athari zitokanazo na janga hilo huku akieleza ofisi yake imeendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu namna bora ya kukinga na maafa pindi yanapotokea.

“Ofisi yetu imeendelea kuelimisha umma kuhusu masuala ya majanga mbalimbali, nitoe rai kwa wananchi kabla ya janga halijatokea pokea elimu ambayo imekuwa ikitolewa na Jeshi la zimamoto kupitia askari wetu wanaopita milango kwa milango ili janga linapokea unakuwa na mbinu za kukabili pia taarifa zitolewe mapema kupitia namba 114 ni namba ya dharura na ni bure, tutakufikia na kukupoa huduma,” alisema Mangale

=MWISHO=