Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Makatibu Wakuu wakutana kujadili hali ya upatikanaji wa mafuta


Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Dkt. Jim Yonazi, ameongoza kikao cha Makatibu Wakuu kilicholenga kujadili hali ya upatikanaji wa mafuta nchini, hususan petroli na dizeli.

Kikao hicho kilichofanyika katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Jijini Dodoma, kimejadili kwa kina changamoto zinazoikabili sekta ya mafuta pamoja na hatua zinazoweza kuchukuliwa ili kuhakikisha upatikanaji wa nishati hiyo muhimu unaendelea kuwa wa uhakika.

Aidha, kikao hicho kilipokea na kuchambua taarifa ya kitaalamu kuhusu hali ya soko la mafuta, ikiwemo athari za mabadiliko ya kimataifa yaliyotokana na vita ya Iran, ambayo imeathiri mwenendo wa upatikanaji na bei za mafuta.

Washiriki wa kikao hicho walisisitiza umuhimu wa kuimarisha mikakati ya kitaifa ya kukabiliana na changamoto hizo, ikiwa ni pamoja na kuimarisha usimamizi wa akiba ya mafuta na kuongeza ufanisi katika mifumo ya usambazaji.

Serikali imeendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa soko la mafuta duniani ili kuchukua hatua stahiki kwa wakati, kwa lengo la kulinda uchumi wa nchi na kuhakikisha huduma muhimu zinaendelea kutolewa bila usumbufu.

 

=MWISHO=