Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Majaliwa: utekelezaji wa mipango ya kilimo upewe kipaumbele


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Fedha na Mipango ihakikishe inaweka kipaumbele cha utekelezaji wa Mipango ya Maendeleo ya Kilimo ya Wilaya (DADPs) ikiwa ni pamoja na kutafuta fedha zitakazowezesha utekelezaji wake.

Ametoa agizo hilo leo (Jumatano, Machi 2, 2022) wakati akizindua Mipango ya Maendeleo ya Kilimo ya Wilaya (DADPs) katika ukumbi wa Chuo cha Mipango, jijini Dodoma. Pia amezitaka taasisi za fedha zijipange kutambua hati miliki za ardhi za wakulima kama dhamana ya kupata mikopo.

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amezielekeza Halmashauri zote nchini zihakikishe zinatenga fedha kutoka katika mapato yake ya ndani kwa ajili ya utekelezaji wa Mipango ya Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ya Wilaya.

“Kwa kuwa asilimia kubwa ya rasilimali za utekelezaji wa ASDP II zinalenga kuelekezwa katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa, Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakurugenzi Watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa waongeze usimamizi wa fedha na rasilimali.”

Waziri Mkuu amewaagiza Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakurugenzi Watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa wahakikishe wanawajenga uwezo wa kusimamia utekelezaji wa miradi katika ngazi mbalimbali na kubuni vyanzo vingine vya kupata fedha za kuendeleza miradi ya kuendeleza kilimo.

Mheshimiwa Majaliwa ameiagiza Ofisi ya Rais - TAMISEMI kupitia Halmashauri zote nchini ziendelee kutenga maeneo ili kuwawezesha wananchi kufanya shughuli za kilimo na shughuli nyingine kama vile ufugaji.

“Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Kilimo ziandae na kusimamia utekelezaji wa mkakati madhubuti wa kusimamia utendaji kazi wa maafisa ugani ili kuongeza uzalishaji na tija katika kilimo. Maafisa Ugani wasimamiwe kikamilifu ili kuimarisha huduma za ugani kwa wakulima.”

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Innocent Bashungwa amesema watashirikiana na Wizara za Sekta ya Kilimo kutekeleza Mipango ya Maendeleo ya Kilimo ya Wilaya kwa kutafuta rasilimali fedha na kusimamia kikamilifu matumizi na utekelezaji wake pamoja na kuimarisha mifumo ya kiteknolojia ya habari na mawasiliano katika sekta ya kilimo (TEHAMA) na kuwezesha upatikanaji wa huduma za kifedha.

Waziri huyo ameongeza kuwa lengo kubwa la Mpango wa Kuendeleza Sekta ya Kilimo kwa awamu ya pili ASDP II, ni kuleta mageuzi ya sekta za kilimo, mifugo na uvuvi ili kuongeza uzalishaji na tija kwa ajili usalama wa chakula, kuongeza kipato kwa wakulima na Taifa kwa ujumla. “Lengo hasa ni kupunguza, kama si kuondoa kabisa umasikini.”

Amesema lengo hilo litafikiwa kwa kufanya mageuzi kwa wakulima kutoka kilimo cha kujikimu, kwenda kilimobiashara, kuzalisha kulingana na mahitaji ya soko kwa wakati huo, kuzalisha mazao (mazao/ufugaji/uvuvi) ya kipaumbele katika kanda kwa kuongeza tija na kuzingatia mnyororo wa thamani, na kuimarisha huduma za ugani.”

Waziri Bashungwa amesema watapitia na kuboresha sera, miongozo na mazingira ya biashara za kilimo, mifugo na uvuvi pamoja na kuimarisha miundo na uwezo wa kitalaamu  wa vikundi vya wakulima na vyama vya wazalishaji, wafanyabiashara na wasindikaji wadogo pamoja na kuimarisha uratibu wa sekta katika ngazi zote za utekelezaji, kuwezesha upatikanaji na kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa takwimu katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi.

Naye, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki  amesema wizara yake itatoa miongozo na kusimamia utekelezaji wa mipango hiyo ili kuhakikisha sekta ya mifugo na uvuvi inakua na tija zaidi pamoja na kuongeza mchango katika pato la Taifa.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Exaud Kigahe amesema watahakikisha mipango hiyo inatelekezwa kwa mafanikio ikiwa ni pamoja na kusimamia uzalishaji wa bidhaa bora zenye uwezo wa kushindana katika masoko ya kimataifa.

Naye, Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde amesema Wizara ya Kilimo inaimarisha uratibu katika ngazi za mikoa kwa lengo la kuzijengea uwezo taasisi mbalimbali zinazohusika na maendeleo ya sekta ya kilimo ili ziweze kutekeleza majukumu yake kwa namna nzuri.

Naibu Waziri huyo ameongeza kuwa kwa sasa sekta ya kilimo inatoa ajira kwa wastani wa asilimia 65 ya Watanzania wote na kwa upande mwingine sekta hiyo inachangia zaidi ya asilimia 65 kwa malighafi viwandani. 

Awali, Makamu wa Rais wa Taasisi ya Kuendeleza Kilimo Afrika (AGRA), Apollos Nwafor alisema taasisi yao itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuleta mapinduzi ya sekta ya kilimo ili kuhakikisha Tanzania inazalisha zaidi na kuweza kulisha Bara la Afrika.

Makamu huyo wa Rais wa AGRA alitumia fursa hiyo kuipongeza Serikali kwa jitihada mbalimbali inazozifanya katika kuboresha na kukuza sekta ya kilimo na kwamba ameahidi kuendelea kuwekeza nchini.

Akizungumza kwa niaba ya wakuu wa mikoa walioshiriki katika hafla hiyo.  Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joseph Mkirikiti alisema watasimamia ipasavyo utekelezaji wa mipango hiyo katika maeneo yao na kuleta mafanikio kama inavyotarajiwa.

-End-