Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Majaliwa azindua programu ajira kwa vijana katika kilimo


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezindua mradi wa Building a Better Tomorrow (BBT) unaolenga kuongeza ushiriki wa vijana katika kilimo kwa kuwapatia mafunzo, maeneo ya mashamba, mitaji na kuwaunganisha na fursa za masoko.

“Vijana wetu fursa ni nyingi nchini kwetu, sekta ya kilimo inabeba fursa zaidi ya asilimia 50, kitendo cha wizara kuzindua mpango mkakati wa vijana kuingia kwenye sekta ya kilimo ni mpango unaolenga kuboresha uchumi wa mto mmoja mmoja kuanzia umri wa vijana.”

Mheshimiwa Majaliwa amezindua mradi huo wa Program ya Ajira kwa Vijana kupitia Sekta ya Kilimo leo (Jumatano, Agosti 3, 2022) katika maonesho ya siku kuu ya wakulima Nane Nane yanayofanyika kwenye Viwanja vya John Mwakangale Jijini Mbeya.  

Pia, Waziri Mkuu amewataka vijana wachangamkie fursa zilizopo katika mradi huo ikiwa ni pamoja na kujihusisha na kilimo cha mazao mbalimbali ili waweze kujikwamua kiuchumi.

Akizungumzia kuhusu mitaji, Waziri Mkuu amesema taasisi zote za kifedha zimepewa maelekezo na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kutoa mikopo kwa wajasiriamali wanaojihusisha na kilimo.

Amesema vijana wasihofu kuingia katika kilimo, waende wakachukue maeneo na waanze kulima kulingana ardhi ya eneo husika. “Maafisa Ugani watawaelekeza kanuni bora za kilimo.”

Waziri Mkuu amesema utekelezaji wa mradi huo ni matokeo ya maagizo na maelekezo ya Mheshimiwa Rais Samia ya kuhakikisha vijana wanapata fursa katika sekta mbalimbali za kiuchumi zikiwemo za madini, kilimo na nishati.

Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka wananchi watumie maonesho hayo kujifunza teknolojia bora za uzalishaji wa bidhaa za mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi ili waongeze uzalishaji na tija katika mnyororo wa thamani.

Awali, Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde alisema programu hiyo itakayowahusisha vijana wa nchi nzima itaanzania na mkoa wa Dodoma na Mbeya kwa ajili ya majaribio na wametenga ekari 69,000.

Alisema maeneo hayo yataandaliwa na kusafishwa na Serikali kabla ya kuwapatia vijana. “Pia vijana watapatiwa pembejeo na kuweka mifumo mizuri ya umwagiliaji, lengo ni kutengeneza ajira zaidi ya milioni tatu.”