Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Maadhimisho siku ya UKIMWI Duniani kufanyika Lindi.


Waziri wa Nchi Ofisi Ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene amesema maadhimisho ya siku ya UKIMWI yanatarajiwa kufanyika Mkoani Lindi katika Uwanja wa Ilulu.

Mhe. Simbachawene ametoa taarifa hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu Ngome, Jijini  Dodoma.

Amesema kuwa maadhimisho hayo yataambatana na maonesho ya shughuli mbalimbali kutoka kwa wadau wa UKIMWI zikiwemo  huduma ya upimaji wa hiari wa virusi vya UKIMWI na magonjwa mengine  itakayotolewa kuanzia   Novemba  24 hadi Desemba  01, 2022.

 

“Kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘Imarisha Usawa’ ambayo imetafsiriwa kutoka kauli mbiu ya kimataifa equalize, kaulimbiu hii inahimiza kutilia mkazo uimarishaji wa usawa kutoa huduma za UKIMWI kwa makundi yote ya wananchi na katika maeneo yote ya kijeografia kwa kuondoa vikwazo vinavyoondoa usawa katika kufikia dira ya kutokomeza UKIMWI ifikapo mwaka 2030.”Amesema Mhe. Simbachawene.

 

Pia ameeleza kwamba maadhimisho hayo yatatumika  kutathimini hali halisi na muelekeo wa kudhibiti virusi vya UKIMWI, Kitaifa na Kimataifa pamoja na kuhamasisha viongozi na jamii kuendelea kwa mapambano  ya kudhibiti virusi vya UKIMWI ili  kujumuisha katika mipango yao ya maendeleo.

“Maadhimisho haya yatatumika kama sehemu ya kuwaenzi wahanga wanaoishi na virusi vya UKIMWI na kuwakumbuka wale waliopoteza maisha  kutokana na UKIMWI pamoja na kujali yatima  ambao wametokana  na vifo vilivyosababishwa na ugonjwa huo.

Vilevile  Waziri Simbachawene ameiagiza  Mikoa yote nchini kuandaa na kuadhimisha siku hiyo kwa kushirikiana na wadau wengine katika  Mikoa na katika ngazi ya Wilaya.

“Maadhimisho haya yatatumika kuhamasisha masuala mabalimbali muhimu ikiwemo  utekelezaji wa azimio la umoja wa mataifa  la kutokomeza UKIMWI katika kuhakikisha  afua za kiafya  zinapewa rasilimali za kutosha na mifumo ya kiafya inaimarishwa”Amebainisha.

Aidha amesema kuendelea kuwepo kwa siku hiyo muhimu kutasaidia  upatikanaji wa dawa za kufubaza VVU, kuendeleza utafiti wa kutafuta chanjo, kuimarisha afua za kinga dhidi ya maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI na kuendelea kutekeleza afua za UKIMWI kwa kuzingatia na kuheshimu haki za binadamu.