Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Kiswahili ni fursa ya kiuchumi-Majaliwa


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wito kwa Watanzania kuzungumza na kusoma lugha ya Kiswahili kwa kuwa lugha hiyo ni fursa ya kiuchumi Duniani.

“Kuwa mzawa wa lugha ya kiswahili pekee, unakuwa hujapata fursa ya  kunufaika nacho, muhimu ni kuendelea kujifunza zaidi ili kuwa mahiri, leo hii kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki Kiswahili kinazungumzwa na hata nchi nyingine zimeingiza kwenye mpango wao somo la Kiswahili. ”

Ametoa wito huo leo (Alhamisi Julai 06, 2023) wakati alipofungua maadhimisho ya Siku ya Kiswahili duniani yaliyofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Polisi, Ziwani Zanzibar.

Amesema kuwa Watanzania wananafasi ya kuwa walimu kwenye nchi mbalimbali ambazo zimeingiza katika mitaala yao somo la Kiswahili “Nataka niwaambie Sisi Watanzania tunayonafasi ya kufundisha Kiswahili nje ya nchi, tuitumie vizuri fursa hii, tuamke na tuone nafasi yetu kwenye kuzitumia fursa hizi. ”

Katika Hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amewaagiza Mawaziri wenye dhamana na lugha ya Kiswahili, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mawaziri wa Elimu, kwa pande zote za Tanzania Bara na Zanzibar kuweka mikakati iliyo wazi ya kukuza Kiswahili na kuweka motisha kwa vijana wanaofanya vizuri shuleni

Aidha, amezitaka mamlaka zinazoshughulika masuala ya ajira ikiwemo Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais (Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi) kuhakikisha kuwa wanaandaa na kuratibu mipango ya kutafuta nafasi za kufundisha lugha ya Kiswahili katika mbalimbali ili Watanzania waweze kwenda kutumia fursa hizo.

“Marais Wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan na Dkt. Hussein Ali Mwinyi wamesema mara kadhaa, tuhakikishe Kiswahili kinakuwa na kuwanufaisha Watanzania”

Naye, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Balozi Pindi Chana amesema kuwa lugha ya kiswahili imeendelea kukua kwa kasi duniani ambapo takwimu zinaonesha kuwa takribani watu milioni 500 wanatumia lugha hiyo.

“Kadiri siku  zinavyoenda uelewa na matumizi ya kiswahili yameongezeka, viongozi wetu mmethibitisha kuwa kiswahili ni muhimu mmezungumza lugha hiyo kwenye mikutano mbalimbli kwa kiswahili kuthibitisha Tanzania ni chimbuko la kiswahili”

Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Tabia Maulid Mwita amesema kuwa Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) na Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) yameendelea kuhakikisha yanaweka mikakati mbalimbali ya kubidhaisha lugha ya kiswahili ikiwemo kupeleka kamusi za lugha hiyo kwenye Bhalozi.

“Tutaendelea kusimamia sheria kanuni na miongozi mbalimbali ili kukuza na kuendeza lugha ya kiswahili,  hata ilani ya uchaguzi ya CCM imetuelekeza kuweka mikakati ya kubidhaisha lugha ya kiswahili. ”