Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria yapitisha makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2026/27


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imepitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya bajeti ya kiasi cha 168,540,287,000 kwa mwaka wa fedha 2026/27 ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zilizopo chini ya Ofisi hiyo.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb.) leo katika Ofisi za Bunge Jijini Dodoma mara baada ya wajumbe kujadili na kuridhia makadirio hayo ya bajeti katika kikao kilichohusisha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Menejimenti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Ofisi hiyo, wataalamu  kutoka Idara na Vitengo vya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Awali akiwasilisha Taarifa kuhusu Utekelezaji wa Bajeti ya mwaka wa fedha 2025/26 na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2026/27 mbele ya kamati hiyo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge,Uratibu na Wenye Ulemavu Mhe. William Lukuvi ameishukuru kamati kwa kujadili na kupitisha makadiri ya bajeti hiyo huku akisema Ofisi yake itaendelea kufanya kazi kwa weledi zaidi kwa kuzingatia jukumu la msingi la Uratibu wa Shughuli zote za Serikali.

Ameongeza kuwa, Ofisi ya Waziri Mkuu inaahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Kamati hiyo ikiwa ni pamoja na kutekeleza maoni na ushauri wa kamati.