Habari
Ifanyeni Great Ruaha Marathon iwe ya kipekee-Majaliwa
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka waratibu wa mbio za hisani za Great Ruaha wazifanye ziwe za kipekee zinazokimbiwa ndani ya hifadhi ili kuhakikisha wanaitangaza hifadhi hiyo pamoja na kutoa hamasa kwa jamii kuhifadhi mazingira kwenye vyanzo vya maji vya Mto Ruaha Mkubwa.
Amesema hayo leo (Jumamosi, Julai 06, 2024) wakati akizungumza na wadau mbalimbali walioshiriki kilele cha mbio za “Great Ruaha Marathon 2024” zilizofanyika ndani ya hifadhi ya Ruaha, mkoani Iringa.
“Kupitia tukio hili la leo, tangazeni sana ili kuvutia washiriki wengi zaidi mwakani. Tunataka mbio hizi ziwe za kimataifa, kupitia mbio hizi pia tunataka kukuza utalii katika Nyanda za Kusini.”
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amewataka wadau wa utalii na wakazi wa eneo la hifadhi ya Ruaha washirikiane na Serikali katika kutekeleza mipango ya kuimarisha shughuli za uhifadhi kwenye eneo hilo.
“Niendelee kuwahamasisha wawekezaji wote wajenge hoteli zaidi pamoja na kambi za muda mfupi; Serikali tuendelee kushirikiana na wadau wa utalii, kwetu sisi tunaendelea na ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami pamoja na ujenzi wa uwanja wa ndege hapa Iringa,” amesema.
Mheshimiwa Majaliwa pia ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Bodi ya Utalii ziendelee kuwashirikisha Watanzania wote wakiwemo wanaoishi nje ya nchi kutumia nafasi walizonazo pamoja na fursa zote zitakazojitokeza kutangaza fursa za utalii za hapa nchini.
“Balozi zetu tulishazipa maelekezo ya kuwa na kitengo cha utalii, kwa sasa ni muhimu pia kuwa na kitini kinachoonesha The Great Ruaha Marathon ambayo inakimbiwa Tanzania ndani ya Hifadhi ya Ruaha.”
Mheshimiwa Majaliwa pia ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii ifanye ukaguzi wa mara kwa mara wa maeneo yote yaliyohifadhiwa ikiwemo kuweka alama ili iwe rahisi kwa wananchi kuyatambua na hivyo kupunguza uvamizi na migogoro baina ya Mamlaka za Hifadhi na wananchi kwenye maeneo husika.
Naye, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Danstan Kitandula amesema kuwa idadi ya watalii katika hifadhi ya Ruaha imekuwa ikiongezeka kila mwaka ambapo mwaka 2022/2023 kulikuwa na watalii 16,833 ukilinganisha na wageni 19,323 walioingia hifadhini mwaka 2023/2024 sawa na ongezeko la asilimia 15.
Aidha, amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada mbalimbali za kuboresha sekta ya utalii nchini ikiwemo hifadhi ya Ruaha ambapo kupitia mradi wa uhifadhi wa mazingira kwa ajili ya utalii (REGROW), kiasi cha dola milioni 150 kilitolewa ukiwa ni mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia kwa ajili kutekeleza miradi ya kufungua utalii Kusini mwa Tanzania.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Peter Serukamba amesema kuwa Ofisi ya Mkoa huo inaishi ndoto za Rais Dkt. Samia za kuifanya sekta ya utalii ilete fedha nyingi za kigeni kwenye uchumi wa nchi. “Sisi tunaendeleza kazi aliyoianza yeye na kupitia mbio hizi za Great Ruaha Marathon tunaamini tutafikia malengo hayo.”
Mapema, Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Huruma Anyagile alisema kuwa asilimia 45 ya wagonjwa wanaotibiwa katika hospitali hiyo ni wenye magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo moyo, kisukari na kwamba njia mojawapo ya kuzuia matatizo hayo ni kufanya mazoezi.