Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

GPSA yakabidhi mafuta ya dizeli lita 10,000 Hanang


Mkoa wa Manyara Mheshimiwa Queen Sendiga aushukuru uongozi wa  Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA) kwa msaada wa mafuta ya Dizeli lita 10,000 waliotoa mapema Disemba 10, 2023 kwa lengo la kuendelea kurahisisha upatikanaji wa nishati hiyo inayohitajika kwa wingi kusaidia zoezi la uendeshaji mitambo na magari yanayotumika kusomba tombe katika maeneo yaliyoathirika na Maafa ya maporomoko ya tope na mawe katika Halmashauri ya Hanang’ mkoani manyara.

Eneo hilo, lilikumbwa na maafa hayo Disemba 3, 2023 na kuleta madhara makubwa ikiwemo vifo, majeruhi, upotevu wa mali na uharibifu wa miundombinu.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi ameendelea kutoa wito kwa wadau kuungana na jitihada zinazoendelea kwa kuchangia vifaa mbalimbali ikiwemo vya ujenzi ambavyo kwa sasa ni hitaji muhimu ili kusaidia wathirika hao.

“GPSA mmefanya kazi nzuri ya kutoa mafuta hayo hakika yatasaidia kwa matumizi ya mitambo na magari yaliyopo site katika zoezi kubwa la kuondoa tope katika maeneo yote na hii niendelee kutoa wito kwa wengine pia kuendelea kuchangia mahitaji mbalimbali yaliyopo hapa Hanang ikiwemo vifaa vya ujenzi, mavazi, vyakula na mahitaji mengine muhimu kwa ndugu zetu  waliofikwa na maafa haya,” alieleza Dkt. Yonazi

Akikabidhi msaada huo Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Masoko wa Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA) Bw. Peter Lukuba amesema msaada huo wa lita 10,000 za mafuta ya dizeli una thamani ya TZS. 34 Mil. na kueleza kuwa wataendelea kutoa mchango wao kwa kuzingatia mahitaji yaliyopo.

=MWISHO=