Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Dkt. Yonazi aishukuru Redcross kwa misaada kwa waathirika wa maafa Hanang’


Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi ameushukuru uongozi wa Taasisi ya Tanzania Red Cross Society kwa namna wanavyoendelea kujitolea na kutoa misaada mbalimbali kwa waathirika wa maafa ya maporomoko ya tope na mawe yaliyotokea Wilayani Hanang’ Mkoani Manyara.

Ametoa pongezi hizo wakati akizungumza na watendaji wa Red Cross walioweka kambi katika Shule ya Katesh A kwa lengo la kuendelea kutoa huduma kama ilivyohitajika kwa kuzingatia kanuni na taratibu zao.

Dkt. Yonazi amesema Serikali inatambua na kujali mchango wao kwa namna walivyojitoa katika kusaidia waathirika wa tukio hilo huku akitoa rai kwa wadau wengine kuendelea kuunga mkono jitihada hizo katika kuwahudumia mahitaji waliyonayo.

Aliongezea kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha wananchi hao wanakuwa katika mazingira mazuri na kuendelea na shughuli zao za uzalishaji kwa utulivu kama ilivyokuwa awali.

“Red Cross mmeendelea kuwa sehemu ya zoezi hili kubwa la kusaidia na kurejesha hali za ndugu zetu huku Hanang’ kwa niaba ya Serikali yetu tunawashukuru sana kwa michango yenu ya hali na mali mliotoa, asanteni sana,” alisisitiza Dkt. Yonazi

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Maendeleo ya Tanzania Red Cross Society Bw. Reginald Mhango amesema kuwa wataendelea kuungana na Serikali katika kila hatua kuona namna wanavyorejesha hali na kusaidia jamii ya wana Hanang’ waliofikwa na maafa hayo.

 

=MWISHO=