Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Dkt. Mwigulu ataka asilimia 20 ya mapato ya mazao ielekezwe kujenga maghala


WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema asilimia 20 ya mapato yatokanayo na mazao ya kilimo inapaswa kuelekezwa katika ujenzi wa maghala karibu na maeneo ya uzalishaji ili kupunguza gharama kwa wakulima na kuongeza ufanisi wa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala nchini.

“Asilimia 20 ya mapato yanayotokana na mazao ya kilimo inapaswa kuelekezwa katika ujenzi wa maghala kwenye maeneo ya uzalishaji ili wakulima wasipate shida ya kusafirisha mazao yao umbali mrefu,” amesema.

Waziri Mkuu amesema hayo leo Mei 19, 2026 alipokuwa mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya miaka 20 ya Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) yaliyofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre jijini Dodoma, yenye kaulimbiu isemayo “Mfumo Imara, Uchumi Endelevu.”

Katika hafla hiyo, Waziri Mkuu pia alizindua rasmi Mkakati wa Uhamasishaji wa Matumizi ya Mfumo wa Stakabadhi za Ghala unaolenga kuongeza uelewa na ushiriki wa wakulima, wafanyabiashara, vyama vya ushirika, taasisi za fedha pamoja na wadau wengine katika matumizi ya mfumo huo nchini.

Dkt. Mwigulu amesema Serikali itaendelea kuimarisha mfumo huo kwa kuwa umechangia kuongeza uwazi na ushindani katika biashara ya mazao pamoja na kuhakikisha wakulima wananufaika na thamani halisi ya mazao yao.

“Pale ambapo kuna changamoto, mbadala wake si uholela. Mbadala wake ni kushughulikia changamoto zinazojitokeza,” amesema.

Aidha, amesema changamoto ya umbali wa maghala haitatatuliwa kwa kurejesha mifumo isiyo rasmi ya biashara ya mazao bali kwa kujenga maghala karibu na maeneo ya uzalishaji.

“Jawabu la changamoto ya umbali wa maghala si kurejesha uholela. Jawabu ni kujenga maghala karibu na wananchi ili wakulima wasipate shida ya kusafirisha mazao yao umbali mrefu,” amesema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali kwa kushirikiana na taasisi za fedha inaandaa utaratibu wa kuwawezesha wakulima kupata malipo ya awali kupitia mazao yaliyohifadhiwa ghalani ili kuwaondoa katika changamoto ya kukopwa mazao au kuuza kwa hasara.

Pia amesema Serikali inaendelea na maandalizi ya mabadiliko ya sheria yatakayoruhusu mali zinazohamishika kutumika kama dhamana ikiwemo stakabadhi za ghala.

“Tunataka stakabadhi ya ghala iwe dhamana inayoweza kumwezesha mkulima kupata fedha wakati akisubiri bei nzuri ya mazao yake,” amesema.

Kadhalika, Waziri Mkuu amesisitiza matumizi ya vipimo rasmi na vifungashio vinavyokidhi viwango huku akieleza kuwa matumizi ya “lumbesa” hayapaswi kuendelea katika biashara ya kisasa ya mazao.

“Lumbesa ni jambo la zamani. Ni namna ya kumwibia mzalishaji mbele ya macho yake. Tuachane nalo,” amesema.

Aidha, amezitaka taasisi za fedha kurahisisha upatikanaji wa mikopo midogo kwa wakulima, wafugaji na wafanyabiashara wadogo ili waweze kutumia huduma rasmi za kifedha badala ya kukimbilia mikopo isiyo rasmi yenye madhara.

Waziri Mkuu amesema Serikali itaitisha kikao cha kitaifa kwa njia ya mtandao kitakachoshirikisha mikoa na wilaya zote kwa lengo la kufanya tathmini ya utekelezaji wa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala na kupokea mapendekezo ya namna bora ya kuondoa changamoto zinazojitokeza katika maeneo mbalimbali.

Awali, Waziri wa Viwanda na Biashara, Bi. Judith Kapinga amesema mafanikio ya miaka 20 ya Mfumo wa Stakabadhi za Ghala yametokana na uwekezaji na usimamizi madhubuti unaoendelea kufanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya WRRB, Bi. Geraldine Rasheli amesema mfumo huo umeendelea kuwa nyenzo muhimu ya kuimarisha biashara ya mazao, kuongeza uwazi wa masoko na kuwawezesha wakulima kupata bei zenye tija.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Mhe. Deodatus Mwanyika amesema Bunge litaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha mfumo huo unakuwa chachu ya maendeleo ya sekta za uzalishaji nchini.