Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Dkt. Biteko afurahishwa na utatuzi changamoto za ardhi Monduli


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewapongeza viongozi wa hal smashauri ya Wilaya ya Monduli kwa jitihada zao za kutatua migogoro ya ardhi wilayani humo ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Serikali kwa viongozi kutatua changamoto za wananchi katika maeneo yao.

Dkt. Biteko ametoa pongezi hizo leo Aprili 23, 2025 wilayani Monduli, mkoani, wakati akihutubia wananchi mara baada ya kukagua miundombinu ya shule Mpya ya Sekondari ya Migungani iliyopo wilayani humo.

“Naomba kuwapongeza tena viongozi wa Wilaya ya Monduli kwa kuendelea kufanya kazi nzuri sana hapa wilayani kwa maslahi mapana ya wananchi wa Monduli. Nimejulishwa kuwa, mmefanya mengi mno ikiwemo utatuzi wa changamoto na migogoro ya ardhi hapa wilayani. Nimejulishwa kuwa sehemu kubwa ya changamoto hizi mmefanikiwa kuzitatua hongereni sana,” amesema Dkt. Biteko.

Ameipongeza pia kamati ya kutatua kero za wananchi inayoongozwa na Mkuu wa Wilaya, ikiwa na wataalamu mbalimbali ambayo imejiwekea utaratibu wa kupokea kero kutoka kwa wananchi na kuzipatia ufumbuzi, ambapo ameitaka pia iratibu zoezi la kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala ya ardhi.

Akiwa shuleni hapo, Dkt. Biteko amewapongeza wananchi kwa kujenga shule hiyo ya Sekondari Migungani ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 85 ya ujenzi huku Serikali ikichangia shilingi milioni 500.

“Sote tunafahamu kuwa, elimu ni msingi mkubwa wa maendeleo. Sisi wana Monduli tayari tunayo shule yetu hii ambayo imeshakamilika. Hii ni miongoni mwa shule zilizopo Wilayani hapa ambazo zitaendelea kutupatia elimu kwa vijana wetu,” amesema Dkt. Biteko.

Ameongeza kuwa Shule hiyo itakuwa na uwezo wa kuchukua wananfunzi 400 na hivyo amewataka wanafunzi kutunza miundombinu na kujifunza kwa bidi ili wajiandae kuwa wazalendo na raia wema huku wakiwa na uwezo wa kutafuta majibu ya matatizo watakayokumbana nayo.

Kuhusu miradi ya umeme wilayani humo, amesema kuwa mwaka huu Serikali inatarajia kujenga mradi mkubwa wa umeme kuboresha upatikanaji wa umeme wilayani humo.

Aidha, Dkt. Biteko amezungumzia maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano kwa kuwataka Watanzania kuenzi muungano huo kwa kujenga Taifa moja kwa kushikamana  na kufanyakazi kwa pamoja kwa kushirikiana.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Mhe. Festo Kiswaga amesema kuwa Wilaya hiyo ni tegemeo kwa Chama Cha Mapinduzi na wamekuwa wakishirikiana na wananchi katika kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo.

Pia, amesema Serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo barabara, hospitali, shule na kuwa Wilaya hiyo ni kati ya wilaya zinazofanya vizuri katika elimu na huku akiumshukuru Rais Samia kwa kuwekeza katika elimu nchini.

MWISHO