Habari
DED Same Atoa Wito Wananchi Kuhama Maeneo Hatarishi
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Same Bw. Jimson Mhagama amewataka wananchi wanaoishi maeneo hatarishi kuhama maeneo hayo ili kuweza kuepuka na madhara ya mvua za El niňo.
Bw. Mhagama ameyasema hayo leo Octoba 05, 2026 Wilayani Same wakati akifungua kikao kazi cha kamati za usimamizi wa maafa za wilaya sambamba na kuimarisha utoaji wa matumizi ya taarifa za tahadhari za awali katika kujiandaa na kukabiliana na madhara ya El nino.
“Tulipitia Kata 34, kati ya kata hizo Kata 20 ndio zenye changamoto katika halmashauri yetu, kati ya kata hizo Kata ya Miamba ndio yenye changamoto zaidi kwa kuwa ardhi ya maeneo yale inatabia ya kuhama/inatembea na ni maeneo hatarishi, pia Kata ya Chome tumeshawaeleza wananchi wa maeneo yale kuhama, mpaka sasa Kaya 10 zimeshahama bado Kaya nne hivyo nawasihi wahame ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza” amefafanua Bw. Mhagama
Aidha, Mkurugenzi huyo amewataka wananchi wa Halmashauri ya Same kuendelea kusafisha mitaro iliyopo katika maeneo yao ili kuweza kujiepusha na madhara yanayoweza kutokea wakati wa mvua hizo.
Kwa upande wake, Mwakilishi kutoka Shirika la Chakula Duniani (WFP) Bi. Sandra Hakim amesema kuwa, Shirika la Chakula Duniani linalengo la kuokoa na kuendeleza maisha ya wananchi na jamii kwa ujumla hasa katika kipindi hiki cha kuelekea ujio wa mvua za El nino zinazotarajiwa kuanza hivi karibuni.
“Tunafurahi kujumuika hapa kwa ushirikiano wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge Uratibu na Wenye Ulemavu), Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) pamoja na Hamashauri ya Wilaya ya Same, lakini pia leo tunafurahi kuwa hapa ili kusambaza taarifa za hali ya hewa kutoka ngazi ya taifa mpaka ngazi ya vijiji ikiwa na lengo la wananchi wa chini kuelewa taarifa za hali ya hewa ili kuweza kujiandaa kabla ya madhara kutokea” ameeleza Bi. Sandra.
Bi. Sandra ameongeza kuwa, taarifa za hali ya hewa za mapema zitakuwa na thamani pale utakapochukua hatua kabla ya majanga kutokea hivyo lengo la programu hiyo ni kuifanya Mamlaka ya Hali ya Hewa kushuka chini ili jamii ikiwemo wazee, wamama, walemavu na Watoto waweze kupata taarifa kwa wakati.
Kikao kazi kimewashirikisha wataalamu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge Uratibu na Wenye Ulemavu), Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) pamoja na Shirika la Chakula Duniani kilicholenga kuimarisha uelewa, utayari na uwezo wa kamati pamoja na timu za wataalamu katika kutekeleza majukumu ya kujiandaa na kukabiliana na maafa.
=MWISHO=




