Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Bajeti ya Serikali imefuta tozo zaidi ya 200 kwa Wafanyabiashara nchini


Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kikundi Kazi cha Maboresho ya Mazingira ya Biashara nchini, Dkt. John Jingu amesema Bajeti ya Serikali imefuta Tozo 232 ambazo zilikuwa changamoto kubwa kwa Wafanyabiashara kwenye Sekta mbalimbali nchini.

Akizungumza na Waandishi wa Habari tarehe 20 Julai, 2022 Jijini Dar es Salaam katika Kikao kazi cha Wadau wa Sekta Binafsi na Watendaji kutoka Taasisi mbalimbali za Serikali, Pia Dkt. Jingu amesema Sheria na Kanuni mbalimbali zaidi ya 40 zimefanyiwa marekebisho ili kuhakikisha mazingira ya biashara nchini yanakuwa mazuri na bora.

“Bajeti imekuwa nyenzo muhimu kuboresha mazingira ya biashara nchini, kwa kiwango kikubwa Bajeti ya Serikali imeweza kushughulikia changamoto mbalimbali za biashara nchini”, amesema Dkt. Jingu.

Amesema mategemeo makubwa, Uchumi wa nchi utakuwa kwa kasi na Wafanyabiashara biashara hao kuchangamkia fursa ambazo zimetengenezwa na Serikali kupitia mifumo ya kikodi, Pia kuongezeka kwa Uwekezaji katika biashara mbalimbali kama biashara ya Mafuta.

Naye, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Dkt. Godwill Wanga amesema punguzo lolote la Kodi, limepunguza gharama za kufanya biashara na kuendelea kukuza uwekezaji nchini.

“Maboresho ambayo yamefanyika kupitia Bajeti ya Serikali ni kwamba Kodi, Tozo mbalimbali zimepungua na imesaidia sana kuuza Uwekezaji nchini na Biashara kwa ujumla, bei za bidhaa zinapungua na Walaji wataongezeka kwa sababu bei imepungua”, ameeleza Dkt. Wanga.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Paul Makanza amesema Wadau wa Sekta hiyo wanahakikisha wanaongeza kasi ya mazingira ya bidhaa nchini na kuchangia ukuaji wa Uchumi.

“Tumetoka kwenye athari za UVIKO-19, pia kuna Vita kati ya Urusi na Ukraine, sehemu mbalimbali duniani kumekuwa na athari za uzalishaji na usambazaji wa bidhaa haujawa mzuri hivyo kuongeza gharama. Hata hivyo Serikali kwenye Bajeti yake, ushuru na baadhi ya Malighafi zimepunguzwa”, amesema Makanza.

 

=MWISHO=