Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Wenye ulemavu wa ngozi kunufaika na mfuko wa ulemavu nchini – Naibu Waziri Nderiananga


Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge Uratibu na Wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga, amesema Watu wenye Ulemavu wa Ngozi wapo Mbioni kunufaika na Mfuko wa Wenye Ulemavu wa Ngozi kwa kupata mafuta maalum kwa matumizi ya ngozi.

Ameyasema hayo Bungeni Jijini Dodoma leo katika Bunge la 13 mkutano wa pili kikao cha nne, wakati akijibu swali la nyongeza lililoulizwa na Mhe. Stella Ikupa Alex (Mb) Viti Maalum CCM lililohoji  ni lini Serikali itatoa mafuta ya watu wenye ulemavu wa ngozi katika Halmashauri nchini.

Mhe. Nderiananga amesema kuwa, Serikali inatambua uhitaji wa mafuta kwa watu wenye ulemavu wa ngozi nchini na kufafanua kwamba kwa kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, kupitia mfuko wa wenye Ulemavu nchini serikali imetenga fedha maalum  na kuzielekeza Kilimanjaro Catholic Medical Centre (KCMC) ili kuweza kuzalisha mafuta mengi zaidi na kuyasambaza.

Aliongeza kuwa, kupitia Wizara ya Elimu, Serikali inasamabaza mafuta hayo ili kuweza kuwafikia wanafunzi wenye ulemavu wa ngozi na yananunuliwa kama vifaa saidizi.

“Tuna hospitali teule kama vile Bugando yanafanyika matibabu hayo ya kufanya uchunguzi wa ngozi kwa ajili ya kutambua aina ya ngozi kwa watoto ili kuwapatia matibabu sahihi na Serikali ina lengo la kusambaza huduma hizo mpaka vijijini” amefafanua.