Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Watanzania wahimizwa kuchangamkia fursa ujenzi wa uwanja mpya wa AFCON Arusha


Watanzania wameaswa kuchangamkia fursa mbalimbali za kiuchumi zinazotokana na ujenzi wa uwanja mpya wa mpira wa miguu unaoendelea kujengwa Jijini Arusha kwa ajili ya michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2027.

 Wito huo umetolewa leo, na Mwenyekiti wa Kamati ya Makatibu Wakuu, ambaye pia ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Dkt. Jim Yonazi, wakati wa ziara ya kamati hiyo ya kukagua maendeleo ya mradi huo unaoendelea Jijini Arusha.

 Akizungumza baada ya ziara hiyo, Dkt. Yonazi ameeleza kuridhishwa na kasi ya ujenzi huo ambao kwa sasa umefikia asilimia 74, huku akisisitiza kuwa uwanja huo ni uwekezaji wa kimkakati utakaoleta tija kwa taifa hata baada ya kumalizika kwa mashindano hayo.

 "Ujenzi huu umefikia hatua nzuri na utakamilika kwa wakati, niwaombe Watanzania wachangamkie fursa zinazojitokeza sasa wakati wa ujenzi na hata baada ya kukamilika kwani uwanja huu utaendelea kutumika kwa mashindano ya ndani na kimataifa," amesema Dkt. Yonazi.

 Aidha, Dkt. Yonazi amebainisha kuwa, usimamizi wa mradi huo unazingatia viwango vya juu vya ubora, ikiwemo kuweka miundombinu rafiki kwa watu wenye mahitaji maalum, ili kuhakikisha huduma zote zinapatikana kwa usawa kwa wageni na wenyeji watakaotembelea eneo hilo.

 Uwanja wa Arusha ni miongoni mwa miundombinu muhimu inayotayarishwa na Serikali ya Tanzania, ambayo ni mshiriki mwenza katika uenyeji wa michuano ya AFCON 2027, ikishirikiana na nchi za Kenya na Uganda.

 Kukamilika kwa uwanja huo kunatarajiwa kuchochea ukuaji wa sekta ya utalii wa michezo jijini Arusha, kutokana na nafasi ya jiji hilo kama kitovu cha utalii katika Ukanda wa Afrika Mashariki.