Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Waziri Mkuu: Serikali imetoa mikopo ya sh. bilioni 1.88 kwa vijana


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana imetoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 1.88 kwa ajili ya kuwezesha miradi 85 ya vijana katika sekta za kilimo, viwanda na biashara kwenye halmashauri 28.

“Ni ukweli usiopingika kuwa suala la uwezeshaji wa vijana ni muhimu katika kukuza uchumi. Hii ni kutokana na ukweli kwamba vijana ni nguvu kazi inayotegemewa na ni kundi kubwa katika nchi yetu. Kwa msingi huo maendeleo yetu yanategemea sana vijana kwani hili ni kundi kubwa na muhimu lenye umri wa kufanya kazi. Wingi wa vijana wenye ujuzi, ni chachu ya kuharakisha maendeleo endelevu,” amesema.. 

Amesema hayo leo Jumapili (Aprili 16, 2023) wakati akizindua Mradi wa Kuwezesha Vijana Kielimu na Kiuchumi kupitia KCB 2jiari wa KCB Foundation na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Ujerumani (GIZ) katika ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wote zikiwemo taasisi za kifedha, mashirika ya kimataifa na sekta binafsi katika kujenga nguv ukazi yenye ujuzi itakayoshiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya Taifa.

“Serikali kwa upande wake inaendelea kutekeleza mikakati na programu mbalimbali za uwezeshaji wa vijana ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kuwekewa mazingira mazuri na wezeshi ya kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo,” amesema. 

Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa tangu ianze kutekeleza Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi, Serikali imetoa fursa za mafunzo ya ujuzi wa kujiajiri au kuajiriwa kwa vijana 118,415 katika fani za uanagenzi, uzoefu wa kazi, ufugaji wa samaki na viumbe maji na kilimo cha kisasa kwa njia ya vizimba. 

Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amewataka vijana waendelee kujitokeza kwa wingi na kuchangamkia fursa za uwepo wa mradi mbalimbali ya kuinua vijana kiujuzi na kiuchumi.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Prof. Joyce Ndalichako amesema kuwa mradi huo ni muhimi kwa kuwa unagusa moja kwa moja vijana ambao ni moja ya nguzo muhimu ya maendeleo ya Taifa.

“Mradi huu wa kuwainua vijana kiuchumi na kiujuzi tukiutekeleza ipasavyo, tutakuwa tumeinua Taifa kimaendeleo na kuimarisha uchumi wa Taifa letu”

 Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya KCB, Cosmas Kimario amesema lengo la mradi huo wa ‘2Jiajiri’ ulioanzishwa mwaka 2000 ni kuboresha ajira na biashara kwa wanawake na vijana nchini na kupunguza mawazo ya vijana kuajiriwa.  

 “Kupitia mradi huu vijana na wanawake, 1,780 wamenufaika na kwa mwaka huu tunatarajia kufikia vijana takriban 5,000,” amesema.