Habari
Waziri Mkuu: Serikali imeongeza wigo huduma za watoto wachanga
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imefanya mageuzi makubwa kwa kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma kwa watoto wachanga.
“Serikali imekuwa ikitekeleza mikakati na afua mahsusi za kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora kwa watoto wachanga. Ni jambo la fahari sana kuwa hivi sasa huduma maalum za watoto wachanga na ile ya Mama Kangaroo hadi kufikia Julai 2024, zimeanzishwa katika hospitali 245,” amesema.
Ameyasema hayo leo (Jumamosi, Septemba 7, 2024) wakati akizungumza na viongozi na wadau walioshiriki mbio za hisani za 2024 zilizoandaliwa na Benki ya Maendeleo (Maendeleo Bank Marathon 2024) katika viwanja vya Green Park, Oysterbay, jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu amesema mafanikio hayo yametokana na dhamira ya dhati ya Serikali ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha Tanzania inapunguza vifo vya watoto wachanga kufikia lengo namba tatu la Maendeleo Endelevu la vifo chini ya 12 katika kila vizazi hai 1,000 kwa mwaka 2030 kutoka vifo 24 kwa kila vizazi hai 1,000 kwa mwaka 2022.
Akizungumzia kuhusu kaulimbiu ya tukio hilo ambayo ni Hatua ya Faraja - Msimu wa Pili, Waziri Mkuu amesema kaulimbiu yao inasawiri mpango wa Benki hiyo wa kuendeleza kazi yao ya mwaka jana ya ununuzi wa vitanda maalumu vya kutunzia watoto njiti (Infant Baby Warmer) katika Hospitali ya KCMC na ujenzi wa kituo kipya cha watoto wenye changamoto ya ulemavu wa akili na usonji kinachotarajiwa kujengwa wilayani Bagamoyo
“Kama mlivyosikia, pale KCMC, idadi ya vifo vya watoto wanaozaliwa njiti ni kubwa na ipo kati ya asilimia 20 mpaka 25. Hawa ni binadamu wenzetu wanaostahili kuishi na tuna kila sababu ya kuonesha upendo kwa kuchangia hatua za faraja. Hivyo basi, nitoe wito kwa wananchi wote wenye mapenzi mema kuendelea kuiunga mkono Benki ya Maendeleo katika utekelezaji wa afua hizi muhimu,” amesisitiza.
Amewapongeza viongozi wa benki hiyo kwa kuongeza lengo la uchangiaji kwenye mbio za mwaka huu kutoka sh. milioni 120 hadi sh. milioni 200 ili kukamilisha kazi waliyoianza mwaka jana
Kuhusu mchango wa madhehebu ya dini, Waziri Mkuu amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa wadau wa sekta binafsi katika kutoa huduma za jamii zikiwepo zinazohusu sekta ya afya, elimu, maji na nyinginezo.
“Ninawapongeza sana Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania kwa kutoa eneo kubwa zaidi kwa ajili ya ujenzi wa kituo kipya cha watoto wenye changamoto ya ulemavu wa akili na usonji. Nimeelezwa kuwa kituo hicho kitajengwa eneo la Kitopeni, Wilayani Bagamoyo ili kukidhi mahitaji ya sasa ya jamii.”
Aliwapongeza viongozi wa Benki ya Maendeleo kwa kufanikiwa kuongeza hadhi ya leseni ya uendeshaji kutoka kuwa Benki ya Kanda (Community Bank) na kupandishwa hadhi ya kuwa Benki ya Biashara ya Kitaifa (Fully-fledged Commercial Bank) kwani hatua hiyo inawaruhusu kufungua matawi nchi nzima.
“Pia ninawapongeza sana kwa ubunifu kwa kuanzisha huduma mbalimbali kama vile mikopo ya nishati mbadala, mikopo ya rasimisha ardhi, mikopo ya bajaji na bodaboda kwa vijana na mikopo ya biashara kwa wamachinga (Wezesha Machinga). Nimeambiwa kwa kushirikiana na uongozi wa Wamachinga, mmebuni mradi mliouita MACHINGA HOUSE- SAMIA CITY unaojumuisha zaidi ya viwanja 500 na zaidi ya ekari 90 katika Kijiji cha Magoza kilichopo Bagamoyo ambapo wamachinga zaidi ya 500 watanufaika na mikopo hiyo katika awamu ya kwanza.”
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel alisema Serikali imeendelea kuisaidia hospitali ya KCMC kwa kuipatia fedha za dawa na vifaa tiba. “Katika ziara yake, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alienda kuzindua jengo la kansa na akaelekeza shilingi bilioni tano zipelekwe kwenye hospitali hiyo.”
“Hadi sasa, shilingi bilioni tatu zimeshatolewa, shilingi bilioni moja itatumwa ndani wiki mbili zijazo na shilingi bilioni moja iliyobakia itatumwa kabla ya Januari, 2025. Pia magari mawili mapya ya kubebea wagonjwa, yataletwa kabla ya Oktoba, mwaka huu,” alisema.
Mapema, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Maendeleo Bank, CPA Peter Tarimo, alisema msukumo wao wa kurudi kusaidia kituo cha Mtoni Diakonia umetokana na uhitaji mkubwa uliopo ambapo kwa sasa kina watoto 107 kutoka pande zote za Tanzania Bara na Zanzibar”ambao wanafundishwa kituoni hapo.
“Watoto wengine 86 wanafikiwa majumbani kwao kupitia programu ya elimu ya majumbani, na wengine 80 wamekosa nafasi ya kujiunga kutokana na uhaba wa miundombinu ikiwemo madarasa na mabweni,” alisema.