Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Waziri Mkuu aunda timu kuchunguza mali za KYECU


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameunda timu maalumu kwa ajili ya kuchunguza mali za Chama Kikuu cha Ushirika wilayani Kyela (KYECU) ili kubaini zilizopo ni kiasi gani.

 “Tunataka kujua mali zilipo na kama kuna zilizochukuliwa tujue ni nani aliyezichukua na kwa nyaraka zipi. Wote watakaobainika kufanya ubadhilifu wa mali za KYECU watachukuliwa hatua.”

 Ametoa taarifa hiyo leo (Jumatatu, Agosti 2, 2021) alipotembelea na kukagua ghala la kuu la KYECU wilayani Kyela akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Mbeya.

Amesema lengo la Serikali ni kuimarisha shughuli za kilimo ili kuona wakulima wakiwemo wa zao la kakao wanapata tija kutokana na shughuli hiyo ikiwa ni pamoja na kunufaika na ushirika.

Pia, Waziri Mkuu amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri za Kyela, Busokelo na Rungwe wahakikishe wanaanzisha vitalu vya miche ya kakao na kuigawa bure kwa wakulima.

Waziri Mkuu amesema hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Septemba mwaka huu halmashauri hizo ziwe tayari zimeshaanzisha vitalu hivyo ili kuwahamasisha wananchi wengi walime kakao.

Kadhalika, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Kilimo ihakikishe wanunuzi wote wa zao la kakao wanawalipa fedha za wakulima ndani ya muda wa saa 48.

Amesema zao la kakao ni miongoni mwa mazao yenye faida kubwa na linazalishwa kwa gharama nafuu, hivyo amewahimiza wananchi kulima zao hilo kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi.

Naye, Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amemuhakikishia Waziri Mkuu kwamba wizaya yao itayasimamia maelekezo yote aliyoyatoa ikiwemo kusimamia kikamilifu kilimo cha zao la kakao.

Amesema Wizara ya Kilimo itapeleka wataalamu katika maeneo yanayolima zao la kakao kwa ajili ya kufanya tathmini ya zao hilo na kubaini changamoto zake ikiwamo magonjwa.

“Tutafufua kitalu cha kuzalisha miche bora ya kakao na kuigawa kwa wakulima na tutaanza kutoa miche 440 itakayomuwezesha kila mkulima kupanda shamba la ukubwa wa ekari moja.”

Awali, Meneja Operesheni wa KYECU, Alid Ndenga aliipongeza Seraikali kwa jitihada zake za kuendeleza ushirika na kusababisha wakulima kupata faida kubwa katika biashara ya zao hilo.

Alisema mfumo wa kuuza mazao kupitia stakabadhi ghalani umekuwa na mafanikio makubwa wilayani Kyela ikiwa ni pamoja na kuimarisha ubora wa kakao na kusababisha bei kupanda.

“Wastani wa bei ya kakao kabla ya kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani ilikuwa kati ya shilingi 2,000 na 3,000 kwa kilo moja, tangu tuanze kutumia mfumo huu bei imeimarika ya chini kabisa ni shilingi 3,700 na imekuwa ikipanda hadi kufikia shilingi 5,787.”

-End-