Habari
Wasaidizi wa Viongozi Wapatiwa Mafunzo ya Mfumo wa Kiongozi App
Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) imeendelea kuimarisha matumizi ya mifumo ya kidijitali Serikalini kwa kuwapatia mafunzo wasaidizi wa viongozi kuhusu matumizi sahihi ya Mfumo wa Kiongozi App.
Mafunzo hayo yamelenga kuongeza ufanisi katika upangaji, uratibu na usimamizi wa ratiba za viongozi mbalimbali wa Serikali ili kuhakikisha shughuli zao zinaendeshwa kwa usahihi na kwa wakati.
Akifungua mafunzo hayo leo tarehe 26 Mei, 2026, Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Uratibu wa Shughuli za Serikali kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw. Paul Sangawe, amesema matumizi sahihi ya mfumo huo yatawezesha kuratibu kazi za viongozi kwa ufanisi na kupunguza changamoto za mgongano wa ratiba.
Bw. Sangawe amewasisitiza wasaidizi hao kuzingatia maelekezo na kutumia mfumo huo kikamilifu ili kusaidia viongozi kutekeleza majukumu yao kwa urahisi na kwa tija.
Aidha, amesema Mfumo wa Kiongozi App umeanzishwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali Mtandao (EGA) kwa lengo la kuimarisha uratibu wa ratiba za viongozi wa Serikali kuanzia ngazi ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mawaziri, Manaibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Manaibu Katibu Wakuu,
Ameongeza kuwa hatua za baadae zinatarajiwa kuhusisha viongozi wa ngazi za juu zaidi akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za Serikali katika kuimarisha matumizi ya TEHAMA na kuongeza ufanisi wa utendaji kazi katika taasisi za umma.




