Habari
Waziri Mkuu akutana na Makamu wa Rais wa Kampuni ya ALSTOM
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amekutana na Makamu wa Rais wa Kampuni ya ALSTOM ya nchini Ufaransa, Philippe Deller ambapo wamejadiliana kuhusu fursa za uwekezaji katika sekta ya miundombinu ya usafiri nchini Tanzania.
Katika mazungumzo hayo, Dkt. Mwigulu Nchemba aliikaribisha ALSTOM kuwekeza nchini, akieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Su Hassan inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji na kutekeleza mageuzi yanayolenga kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara, usafiri na uwekezaji katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Kwa Upande wake Bw. Phillepe alieleza nia ya kampuni hiyo kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya usafiri wa mijini.
Kampuni hiyo imeonesha utayari wa kuwekeza katika ujenzi wa mifumo ya usafiri wa haraka na miundombinu ya kisasa yenye lengo la kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam, huku ikitazama pia fursa za utekelezaji wa miradi kama hiyo katika majiji ya Mwanza, Mbeya na Arusha.
Miradi hiyo inatarajiwa kuongeza ufanisi wa usafiri wa mijini, kupunguza muda wa safari, kuimarisha shughuli za biashara na uwekezaji, pamoja na kuchochea ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya wananchi kupitia matumizi ya teknolojia za kisasa.
Mazungumzo hayo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha ushirikiano na kampuni kubwa za kimataifa ili kuleta teknolojia, utaalamu na mitaji inayochochea maendeleo ya miundombinu na uchumi wa Taifa.
Kampuni ya ALSTOM, ina uzoefu mkubwa katika kubuni, kujenga na kuendesha mifumo ya kisasa ya usafiri wa umma ikiwemo reli za kisasa, treni za mwendo kasi, metro, tram na teknolojia za usimamizi wa usafiri.




