Habari
Wadau wahimizwa kuimarisha ushirikiano katika kuwawezesha watu wenye ulemavu
Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu kupitia Kitengo cha Huduma kwa Watu Wenye Ulemavu imewahimiza wadau kuimarisha ushirikiano na Serikali katika kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata huduma stahiki na fursa za uwezeshaji kiuchumi ili waweze kujitegemea na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo nchini.
Wito huo umetolewa leo na Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma kwa Watu Wenye Ulemavu Bw. Kizito Wambura wakati wa ufunguzi wa kikao kazi kilichowakutanisha Ofisi ya Waziri Mkuu, Shirika la Sense International Tanzania na Chuo cha Ufundi Stadi na Utengamao kwa Watu Wenye Ulemavu cha Sabasaba kilichopo Mkoani Singida kwa lengo la kupokea taarifa ya utekelezaji wa mradi wa kuwawezesha vijana wenye ulemavu kupitia mafunzo ya ufundi stadi.
Bw. Wambura amesema mradi huo ni muhimu katika kuwajengea vijana wenye ulemavu ujuzi na uwezo wa kujitegemea kiuchumi, kwa kuwawezesha kujiajiri au kuajiriwa baada ya kuhitimu mafunzo na kusisitiza umuhimu wa kuimarisha mawasiliano na mtiririko wa taarifa kati ya wadau na Serikali kuhusu shughuli zinazotekelezwa, ili Serikali iweze kufahamu juhudi hizo na kuongeza nguvu pale inapohitajika.
Aidha, amezitaka Sense International Tanzania na Chuo cha Sabasaba kuhakikisha utekelezaji wa mradi huo unaleta matokeo chanya kwa vijana wanaonufaika, hususan katika kuwapatia ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira na kuwawezesha kutumia fursa zilizopo kujikwamua kiuchumi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Sense International Bw. Julius Mahundi, ameishukuru Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu kwa ushirikiano inayotoa katika kuboresha ustawi wa watu wenye ulemavu.
Amesema shirika hilo linatarajia kuwa mradi huo utasaidia kukabiliana na changamoto zinazowakabili vijana wenye ulemavu kwa kuwawezesha kupata elimu, mafunzo, taarifa sahihi na fursa za masoko.
Mradi huo unaotekelezwa kuanzia mwaka 2024 hadi 2027 na Sense International kwa kushirikiana na Chuo cha Ufundi Stadi na Utengamao wa Watu Wenye Ulemavu cha Sabasaba kilichopo mkoani Singida unalenga kunufaisha vijana wenye ulemavu wenye umri wa miaka 15 hadi 35. Mradi huo umefadhiliwa na Farao Island na Hodge International.




