Habari
Utekelezaji wa Dira 2050 uanze-Dkt. Mwigulu
WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba ameagiza kuanza utekelezaji wa Dira 2050 kupitia Mpango na Bajeti iliyoandaliwa na kuendelea kuishirikisha sekta binafsi na wadau wa maendeleo katika kuharakisha utekelezaji wake ili kujenga uchumi jumuishi, shindani na unaotegemea uzalishaji wenye tija.
Aidha, Waziri Mkuu ameilekeza Tume ya Mipango kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu Dira 2050 ili kuwezesha kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wake kwa sababu suala hilo litawezekana ikiwa wadau wote watakuwa na ufahamu wa kutosha kuhusu vipaumbele vilivyoainishwa katika Dira 2050.
Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo (Jumatano, Aprili 1, 2026) wakati akiwasilisha hotuba yake kuhusu Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa Mwaka 2026/2027 Bungeni jijini Dodoma.
Amesema Dira 2050 iliyozinduliwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan mnamo tarehe 17 Julai, 2025, itaongoza mipango ya maendeleo katika miaka 25 ijayo inalenga kujenga Taifa jumuishi, lenye ustawi kwa wote, lenye haki na linalojitegemea.
“Nitoe rai kwa viongozi wa Serikali, Dini, Sekta Binafsi, Asasi za Kiraia na Wadau wa Maendeleo kuhakikisha kwamba mipango yao inawiana na vipaumbele vya Dira 2050 na kuiunga mkono katika utekelezaji wake”.
Amesema utekelezaji wa Dira hiyo, utawezesha Taifa kuwa na uchumi wenye thamani ya dola za Marekani trilioni moja na wastani wa pato la mtu mmoja mmoja kuwa dola za Marekani 7,000 kwa mwaka ifikapo 2050. “Nguzo muhimu za kutuwezesha kufikia malengo hayo ni pamoja na utawala bora, amani, usalama na utulivu.”
Vilevile, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu amewaagiza viongozi wa kila sekta wahakikishe rasilimali zote za Taifa zinaelekezwa katika maeneo yenye tija na matokeo makubwa ili kupunguza utegemezi kutoka nje.
Amesema kuwa Dira 2050 imejengwa na nguzo kuu tatu ambazo ni uchumi imara jumuishi na shindani; uwezo wa watu na maendeleo ya jamii; na uhifadhi wa mazingira na ustahimilivu wa mabadiliko ya tabianchi.
Amesema katika hatua za kutekeleza Dira hiyo kwa vitendo, Serikali kwa kushirikiana na wadau imeweka mikakati mbalimbali ya utekelezaji, ambayo ni pamoja na kuchagiza ubia kati ya sekta ya umma na binafsi.
Waziri Mkuu ameongeza kuwa mikakati mingine ni pamoja na matumizi yenye tija ya rasilimali za Taifa kupitia utekelezaji wa programu za kimkakati na kukuza utamaduni wa kuweka akiba kwa ajili ya uwekezaji.
Amesema Mpango na Bajeti itakayopitishwa na Bunge hilo ni hatua ya kwanza ya utekelezaji wa Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027 - 2030/2031 na Dira 2050,huku dhima ya mpango huo ni “Mageuzi katika Kukuza Uchumi na Kuzalisha Ajira.”
Amesema mipango hiyo inawezesha Taifa kuelekeza rasilimali katika vipaumbele vya kimkakati vyenye matokeo makubwa kwa ajili ya ukuaji wa uchumi na ustawi wa wananchi.
Aidha, Waziri Mkuu amesema kwa kutambua umuhimu wa Dira hiyo, Serikali itaendelea kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji na tathmini pamoja na kuhimiza uwajibikaji, ili kuhakikisha tunafikia malengo tuliyojiwekea.
Waziri Mkuu ameliomba Bunge liidhinishe jumla ya shilingi trilioni 12.50 kati ya fedha hizo, shilingi trilioni 8.73 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi trilioni 3.76 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo. Fedha hizo ni kwa ajili ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake kwa mwaka 2026/2027.
Vilevile, Waziri Mkuu ameliomba Bunge liidhinishe jumla ya shilingi 225,021,780,000 kwa ajili ya Mfuko wa Bunge. Kati ya fedha hizo, shilingi 207,992,798,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi 17,028,982,000 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.




