Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Urasimishaji wa ukalimani wa lugha ya alama wasisitizwa


Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Watu Wenye Ulemavu), Mhe. Ummy H. Nderiananga (Mb), amesisitiza umuhimu wa kuharakisha urasimishaji wa tasnia ya ukalimani wa Lugha ya Alama ya Tanzania, ili kuhakikisha watu wenye ulemavu wa kusikia wanapata huduma kwa usawa.

Akifungua kikao cha mashauriano kilichoandaliwa na Chama cha Viziwi Tanzania (CHAVITA), na kuhudhuriwa na viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA), Wabunge pamoja na wadau mbalimbali, Jijini Dodoma, Mhe. Nderiananga amesema hatua hiyo itasaidia kuweka viwango vya taaluma, kuboresha mafunzo, na kutambua rasmi wakalimani wa Lugha ya Alama nchini.

Aidha, Mhe. Nderiananga amesema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuandaa miongozo na kanuni zitakazosaidia kusimamia taaluma hiyo, huku akihimiza jamii kuongeza uelewa wa matumizi ya Lugha ya Alama, ili kuondoa vikwazo vya mawasiliano.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CHAVITA, Bi. Selina Mlemba amesema, urasimishaji wa tasnia ya ukalimani wa Lugha ya Alama ni hatua muhimu katika kuhakikisha haki za watu wenye ulemavu wa kusikia zinalindwa na kutekelezwa kwa vitendo.

Aidha Bi. Mlemba ameongeza kuwa CHAVITA itaendelea kushirikiana na Serikali pamoja na wadau wengine ili kuhakikisha kunakuwepo na miongozo, mafunzo, pamoja na mfumo rasmi wa usajili wa wakalimani wa Lugha ya Alama nchini, sambamba na hilo amesisitiza kuwa hatua hiyo itachangia kuongeza ubora wa huduma katika sekta mbalimbali na kuwezesha ushiriki kamili wa watu wenye ulemavu wa kusikia katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Washiriki wa kikao hicho wameitaka Serikali kuipa kipaumbele tasnia hiyo, wakisisitiza umuhimu wa ajira kwa wakalimani wa Lugha ya Alama katika sekta zote, pamoja na kuimarisha mafunzo na utambuzi wa taaluma hiyo ili kuboresha huduma kwa watu wenye ulemavu wa kusikia.